Madiwani wa kata zilizo na masoko makubwa matano ya Sido, Mwanjelwa, Soweto, Igawilo na Sokomatola yaliyopo jijini Mbeya wakishiriki kwenye Kikao kazi kilichoandaliwa na Shirika la WeCare Foundation kikiwakutanisha wadau mbalimbali jijini humo kikilenga kuhamasisha Programu ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM). Miongoni mwa mambo yaliyoazimiwa kwenye kikao hicho ni pamoja na kuanzishwa kwa vituo vya kulelea watoto kwenye masoko.(Picha na Joachim Nyambo)
……….
Joachim Nyambo, Mbeya.
WADAU jijini Mbeya wamekuja na azimio la kuanzishwa kwa vituo vya kulelea watoto wadogo hususani walio na umri wa chini ya miaka mitano katika maeneo ya masoko lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya ukuaji wao.
Watoto wadogo wanaoshinda kwenye maeneo ya biashara hususani masoko wanatajwa kuwa hatarini hususani kiafya kutokana na mazingira ambayo wazazi wao wanafanyia biashara kutokuwa rafiki kwao.
Hayo yalibainishwa kwenye Kikao kazi kilichoandaliwa na Shirika la WeCare Foundation kikiwakutanisha wadau mbalimbali jijini hapa kikilenga kuhamasisha Programu ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM).
Miongoni mwa wadau walioshiriki kikao kazi hicho ni pamoja na madiwani kutoka kwenye kata tano zilizo na masoko makubwa jijini hapa, maafisa watendaji pamoja na maafisa maendeleo ya jamii wa kata 36 na pia wenyeviti wa mitaa mitano yalipo masoko ya Sido,Mwanjelwa,Soweto,Igawilo na Sokomatola.
Katika kikao hicho wadau hao walisema kutokana na wazazi kutingwa na shughuli za kibiashara watoto wadogo wamekuwa hawapati malezi stahiki kwani wapo ambao wamekuwa wakiachwa majumbani pasipo uangalizi wa karibu huku wale wanaobebwa sokoni na wao wakiachwa kwenye mazingira yasiyo rafiki ikiwemo kuchezea uchafu hatua inayoweza kuwasababishia magonjwa.
Diwani wa Kata ya Maendeleo lilipo soko la Sokomatola, Issa Salimin alikiri kuwepo kwa changamoto ya watoto wanaoshinda sokoni kukosa malezi stahiki akisema wengi wanaathiriwa na mazingira yasiyo rafiki kwa ukuaji wao.
“Mimi nina soko hapa, ukiangalia changamoto hiyo ni kubwa…utakuta mama anafanya biashara lakini mgongoni ana mtoto mchanga… Tumejifunza kitu na ni muhimu tuwe na vituo ambavyo watoto wa wafanyabiashara watalelewa hapo kwa muda ambao wazazi watakuwa wanaendelea na biashara.” Alisema Salimin.
Naye diwani wa Kata ya Igawilo, Hanada Mdidi alisema ipo haja kwa halmashauri kutenga bajeti maalumu kwaajili ya kuanzisha vituo maalumu kwaajili ya kulelea watoto kwenye masoko ili kuwaepusha na changamoto wanazokutana nazo ikiwemo kulishwa viporo kwa wazazi kukosa muda wa kuwapikia chakula kwa wakati.
“Kwanza mimi mwenyewe ni mama na ninawiwa sana na hawa akina mama wanaoweza kwenda na watoto wadogo kwenye maeneo ya biashara na wale wanaowatelekeza majumbani wanabaki wanahangaika.
Hata kabla ya kikao hiki nimejaribu mara kadhaa kuongea na wanawake wenzangu kuwa tunapofanya biashara tujitahidi sana na kuangalia familia zetu.” Alisema diwani huyo.
Akifungua kikaokazi hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa aliwataka wadau kushirikiana kwa karibu kutekeleza azma ya kuwa na vituo vya watoto kwenye masoko akisema wazo hilo litaisaidia jamii kuwa na watoto wanaopata stahiki zote za malezi yenye muitikio.
Malisa alisema kutokana na uzito wa wazo hilo ni muhimu wadau wakawa na wigo mpana wa utekelezaji wake ili badala ya vituo kuanzishwa kwenye masoko makubwa pekee, masoko madogo nayo yaanzishe ili kutoa huduma hiyo.
Mkurugenzi wa WeCare Foundation, Elizabeth Maginga alisema ni muhimu kwa viongozi kwenye ngazi za kata na mitaa kupata taarifa na uelewa juu ya PJT-MMMAM ili wasaidie wazazi na walezi kujitokeza kupata elimu ya programu hiyo na kushiriki kwenye utekelezaji wake.
Grace Sangu na Eva Shauga ni wafanyabiashara waliokutwa na mwandishi wa habari hizi wakiwa na watoto wadogo katika soko la Sokomatola ambapo walikiri kuwepo na changamoto kubwa ya malezi ya watoto hususani walio na umri wa kutambaa wakati wazazi wakiendelea kuwahudumia wateja.
“Kuanzishwa kwa vituo kutatupa uhakika wa watoto kuwa sehemu salama wakati tukiendelea na biashara. Kwa sasa tunawaacha wacheze na watoto wenzao ambo kidogo wao wanakuwa ni wakubwa. Changamoto ni kubwa kwakuwa kwa umri wao hawawezi kutambua kuwa hizi ni taka wasichezee. Lakini pia tunafanya biashara jirani na barabara hivyo inabidi kuangalia magari huku tukihudumia wateja.” Alisema Grace.
Naye Eva alisema “Mpango huo ni mzuri kwakuwa utatusaidia sisi akina mama tulio na watoto wadogo. Itawezesha wao wakiwa wanaendelea na michezo yao na sisi tuwe kwenye biashara. Tunaomba wazo hili litekelezwe tunao uhitaji mkubwa.”