Dkt. Lihoya Chamwali (Kulia) akikabidhi kompyuta za Mradi wa HEET kwa niaba ya Mratibu wa Mradi huo kutoka Chuo Kikuu Mzumbe. Kompyuta hizo zimepelekwa Ndaki ya Dar es Salaam kituo cha Tegeta. kushoto ni DKt. Janeth Swai aliyepokea kompyuta hizo kwa niaba ya Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam. Makabidhiano hayo yamefanyika Septemba 22, 2023.
Sehemu ya Kompyuta zilizotolewa na Mradi wa HEET zikiwa tayari kwa matumizi katika maabara ya kompyuta Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Kituo Cha Tegeta. Jumla ya kompyuta 70 zimetolewa katika Ndaki hiyo.
Dkt. Lihoya Chamwali akikagua kompyuta zilizotolewa na Mradi wa HEET katika maabara ya kompyuta Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Kituo Cha Tegeta hivi karibuni.
Mwakilishi wa Mradi wa HEET Dkt. Lihoya Chamwali(wapili kushoto)na Mratibu wa Kituo cha Shahada za Awali Tegeta, Dkt. Janeth Swai (Katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam mara baada ya makabidhiano ya Kompyuta 70 kutoka Mradi wa HEET
……
Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salam, Kituo cha Tegeta kimepokea kompyuta sabini (70) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi “HEET – Project” kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kujifunza na kujifunzia hasa kidijitali. Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kuratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akikabidhi Kompyuta hizo Septemba 22, 2023, Kwa niaba ya Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lihoya Chamwali amesema kuwa, lengo la kutolewa kwa kompyuta hizo ni kusaidia wanafunzi kutumia TEHAMA katika masomo yao, shughuli mbalimbali za kitaluma na kukuza ujuzi wa kidigitali utakaoleta tija katika jamii na Taifa.
Akipokea Kompyuta hizo Kwa niaba ya Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam, Mratibu wa Shahada za Awali Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kituo cha Tegeta, Dkt. Janeth Swai ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha upatikanaji wa mradi wa HEET nchini na Chuo Kikuu Mzumbe kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu zinazoendelea kunufaika na mradi huu.
Dkt. Swai amesema upatikanaji wa Kompyuta hizo utasaidia wanafunzi wa Ndaki ya Dar es Salaam kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayohitaji matumizi zaidi ya vifaa vya kidijitali na hivyo kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajirika katika taasisi mbalimbali na hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi kama lilivyo lengo kuu la mradi.