Baadhi ya Maafisa Utumishi na IT wa Serikali wakifuatilia mkutano wa mrejesho wa usajili wa wafanyakazi katika mfumo wa Mfuko wa Huduma za Afya uliofanyika Ukumbi wa Studio Rahaleo
Na Rahma Khamisi Maelezo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar, (ZHSF) Yassir Ameir Juma amewataka wafanyakazi wa Taasisi za Serikali kukamilisha usajili wa huduma za afya kwa haraka ili kupatiwa kadi za uwanachama.
Wito huo ametolewa katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo wakati wa Kikao cha mrejesho wa usajili wa uwanachama wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar kwa Maafisa Utumishi na IT wa Serikali.
Amefahamisha kuwa jumla ya wanachama 26 elfu wameshasajiliwa rasmi ambapo wafanyakazi 20 hawajakamilisha usajili huo hivyo amewahimiza kukamilisha usajili wao ili kuanza kutumia huduma hiyo.
Aidha amesema kuwa Mfuko una haki ya kuhakikisha wanachama wote wamesajiliwa katika mfumo na kupata huduma zote za msingi.
Amesema kwa wafanyakazi walikwisha kamilisha usajili wao watapatiwa kadi zao hivi karibuni.
Kaimu Mkurugenzi ameongeza kuwa kwa wale ambao wameshakamilisha usajili wao watapatiwa ujumbe mfupi kupitia simu zao kuhakikisha usajili wao hivyo kila mtu ahakikishe anapata taarifa zake ili kuwaondeshea usumbufu wanachama wao.
Nae Afisa Tehama kutoka Wizara ya Fedha Muhammed Abdalla Ali amesema kuwa lazima wafanyakazi wote wa serikali wawemo katika mfuko wa huduma ya afya ili kurahisisha kuonekana kadi inapoingizwa katika mfumo huo.
Aidha amefahamisha kuwa katika mfumo huo kutakuwa na invoice ambayo itaonesha kila mfanyakazi na taarifa zake ili kuondosha usumbufu.
“Ikitokea katika mfumo wako kuna watu 20 na invoice yako inaonesha watu 21 hapo utatakiwa kutoa taarifa sehemu husika kwa ajili ya kurekebishiwa,” alifahamisha.
Nao wafanyakazi hao wameuomba Mfuko huo kuwapatiwa taarifa za uhakika pindi watakapokamilisha usajili nili kuweza kutambua kinacoendelea.