Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani kwaajili ya kuhutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
PICHA B2-B03
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Balozi Elsie Kanza (Kushoto) wakati akiondoka katika Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani mara baada ya kuhutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
…………………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kwa sasa dunia inashuhudia kufifia kwa mshikamano thabiti wa kihistoria, udugu na kujitolea, kutoingiliana, usawa baina ya mataifa na kunufaishana uliowekwa na waanzilishi wa Umoja wa Mataifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani. Amesema ili kurejesha imani na mshikamano baina ya mataifa ni vema mataifa yaliyoendelea kuhakikisha yanatimiza ahadi zake na sauti za mataifa yanayoendelea zinasikilizwa.
Amesema kumekuwepo na kutoaminiana baina ya mataifa na hivyo kupelekea mmomonyoko wa utawala wa sheria, mataifa kuunda miunganiko tofauti na ile ya asili pamoja na kurejea kwa maamuzi ya upande mmoja. Ameongeza kwamba kwa sasa kumekuwa na maswali zaidi juu ya ufanisi wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa pamoja na Taasisi za Fedha za kimataifa zikihitajika kufanyiwa maboresho ya haraka.
Makamu wa Rais amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuwakemea kwa uwazi wale wote wanaoshiriki katika kuchochea migogoro barani Afrika kwa lengo la kuuza silaha au kupata utajiri wa rasilimali zilizopo. Ameongeza kwamba dunia inahitaji kuwekeza zaidi katika mazungumzo na diplomasia katika kutatua migogoro ya kivita ili kuifanya kuwa sehemu salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Tanzania itaendelea kuchangia katika juhudi za kuleta na kudumisha amani barani Afrika na kwingineko duniani na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono katika mipango ya kikanda ya kuleta amani katika maeneo yenye vita barani Afrika. Amesema hadi kufikia mwezi machi 2023 Tanzania imekua ndio mchangiaji mkubwa wa 12 kati ya nchi 125 katika shughuli za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.
Makamu wa Rais amesema utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu umekuwa wa kukatisha tamaa hasa kutokana na kutotekelezwa kwa ahadi za kifedha na teknolojia kutoka kwa nchi zilizoendelea duniani na upungufu wa fedha katika nchi nyingi za Afrika.
Amesema Tanzania imedhamiria kutekeleza kikamilifu malengo ya maendeleo enedelevu kama inavyotarajiwa ambapo Julai mwaka huu iliwasilisha Ripoti ya pili ya Hiari ya Taifa (VNR) ambayo inaonyesha kwa ujumla kumekuwa na mafanikio makubwa kwa lengo namba 2 – 7 kwa ongezeko la uwiano wa kutosha wa chakula, upatikanaji wa dawa muhimu, kupungua vifo vya chini ya miaka 5,hatua muhimu katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, uboreshaji wa upatikanaji wa maji mijini na vijijini pamoja na utoaji wa huduma ya nishati ya umeme. Ameongeza kwamba pamoja na kuwepo kwa utendaji wa wastani katika lengo namba 1,8 na 10, Tanzania imedhamiria kuchukua hatua kuboresha zaidi juhudi za mapato ya ndani huku ikitumia mfumo wa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi pamoja na kuweka kipaumbele kwenye uwekezaji katika sekta za huduma za jamii, kilimo na biashara ya kilimo, uongezaji thamani na miundombinu, pamoja na kuinua ujuzi wa vijana.
Kuhusu mazingira, Makamu wa Rais amesema Tanzania inasisitiza wito wake wa kuchukua hatua za haraka na za pamoja za kupunguza uzalishaji wa gesijoto pamoja na kuimarisha hatua za kukabiliana na hali hiyo. Amesema ni lazima kuweka mazingira wezeshi na kuwezesha uwekezaji unaohitajika ili kutumia rasilimali kwa ajili ya kuongeza utekelezaji wa ahadi zinazohusu mabadiliko ya tabianchi na uondoaji wa kaboni katika uchumi wa dunia. Aidha amesema Tanzania inasisitiza wito wake wa mabadiliko ya haki katika kufikia nishati safi kwa nchi za Afrika.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuwa imara katika kupinga dhuluma popote inapotendeka na kwa yeyote yule. Ametoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi visivyo vya haki kwa mataifa kwani vimekua vikidhoofisha uhuru na ustawi kwa wote.