Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga amesema shirika lipo tayari kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya Sita china ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha mradi wa kuunganisha wilaya zote nchini katika mkongo wa Taifa inakalimika.
Hayo ameyasema septemba 21 jijini Dar es salaam wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Khamis Abdalla kufuatilia utekelezaji wa upanuzi wa mkongo wa Taifa.
Amesema upanuzi huo wa awamu ya Tatu utakwenda kwenye wilaya 32 ambapo wilaya 23 ziko chini ya mkandarasi na wilaya 9 ziko chini ya TTCL.
“Mradi huo ni wa upanuzi wa mzunguko wa kaskazini na Magharibi kutoka 800Gbps hadi 2Tbps na ufikishwaji wa mkongo wa Taifa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo”amesema Ulanga
Amesema vifaa ambavyo vitatumika katika mradi huo vinekuja kwa awamu ya kwanza ambovyo ni faiba na vifaa vyake ambapo ifikapo mwisho wa mwezi Oktoba shehena ya vifaa vyote vitakua vimeingia kwa ajili ya awamu 2,3 na 4.
Amesema katika kukamilsh mradi huo timu ya wasimamizi imeandaliwa ambao watakua na jukumu la kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo kikamilifu na kuzingatia weledi.
“Tumewapatia vitendea kazi ikiwemo magari kwa kila msimamizi wa mradi ili kurahisisha shughuli katika kutekeleza Miradi hiyo”ameongeza Ulanga
Amesema ujenzi wa vituo 9 unaofanywa na wataalam wa ndani unaendelea na tayari baadhi ya vituo vya kutolea huduma kama Tarime na Sengerema vinekamilika huku Rujewa na Rorya vipo kwenye hatua ya mwisho.
Amesema ujenzi huo umeshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Tanesco ambao miundombinu Yao inatumiwa kwa pamoja na NICTBB hivyo kutasaidia kufanikisha malengo ya mradi.
Akizungumzia uelewa wa wananchi kuhusu mradi huo amesema wamefanya shughuli mbalimbali za kutoa elimu kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya husika na kamati ya ulinzi na usalama ili kuwajengea uelewa wananchi kuhusu manufaa yanayotokana na mradi.
Akizungumzia kuhusu ufikishwaji wa mkongo wa Taifa katika nchi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema mkandarasi ameshapatikana na mkataba umeshasainiwa hivyo ataanza kazi haraka.