Na Sophia Kingimali
Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji katika mikoa ya Lindi,Mtwara na Pwani ambayo iliwekwa kwenye mpango wa utekelezaji wa 2023/2024 ambao utawezesha umwagiliaji wa mashamba yenye hekta 49,307 kutoka hekta 13,270 za sasa kufuatia ujenzi wa mabwawa 21.
Aidha jumla ya skimu 54 zenye ukubwa wa hekta 88,206 zinafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Hayo yamejili baada ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kukamilisha ziara ya kimkakati ya siku 7 katika mikoa ya Lindi,Mtwara na Pwani.
Serikali imeahidi kutekeleza mkakati wa kuliingiza zao la mbaazi na ufuta katika mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo tayari umeimarisha bei ya mbaazi mpaka kufikia 2300 kwa kilo huku ufuta ukiwa 38000 kwa 4000 kwa kilo.
Sambamba na hayo serikali imetoa wito kwa wakulima kuweka akiba ya fedha.
Rais Dkt Samia amesema serikali inaendelea na usajili wa mikorosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo amezielekeza mamlaka husika kusimamia usafirishaji wa zao hilo.
Amesema sasa zao litasafirishwa kwa Meli ambapo mtu akitaka kusafirisha kwa gari anapaswa kuwa na vibali maalumu lakini pia kuruhusu bandari ya Mtwara kuanza usafirishaji wa zao hilo.
Sambamba na hayo Wizara ya Kilimo imejipanga Kuja na mkakati wa kuliongezea thamani zao la Ufuta na Korosho kwa kuanzisha kungani ya viwanda.
Mpaka sasa serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kongani hiyo katika eneo la Maranje,Nanyamba mkoani Mtwara pamoja na kuanzisha kiwanda cha kubangulia korosho kilichopo Lindi.
Hata hivyo wizara ya kilimo imejipanga kuwezesha wakulima kumudu uzalishaji wa mazao mengine ya Nazi,Ufuta na Mbaazi kwa kugawa mbegu za miche bora na kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao hayo.