*Asema Rais Samia anatamani kuona utekelezaji wa mradi huo uendelee kwa kasi ili kutimiza lengo la kuanzishwa*
*Ataka Mradi huo kuwa wa mfano kupitia mpangokazi kuepuka migogoro*
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameutaka Uongozi wa Mgodi wa Tembo Nickel kuandaa na kuwasilisha Serikalini Mpango Mkakati unaoonyesha namna wanavyoenda kushughulikia eneo lote la leseni ili kuhakikisha wanaepuka migogoro na wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Alisema hayo Septemba 20, 2023 wakati akizungumza na uongozi wa mradi wa Tembo Nickel unaomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Kabanga Nickel, uliopo Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za Sekta ya Madini katika Mikoa ya Kagera na Geita.
“Mradi huu tunataka uwe wa mfano hapa nchini, hatutaki kurudia makosa yaliyotokea huko nyuma kutokana na miradi kuingia kwenye migogoro na wananchi wanaozunguka maeneo yao, nyie muwe mfano katika kuepuka hili kupitia mpango kazi wenu” alisema Dkt. Kiruswa.
Aliwataka kuratibu suala la kuwalipa fidia na kuwahamisha ili kuepuka usumbufu na kwamba wahakikishe wanawalipa fidia kwa awamu ili kusiwe na usumbufu wakati bado hawajahamia katika nyumba wanazojengewa, ili kila mguswa ahamie kwenye nyumba yake akiwa na fedha za kujikimu na kuendeleza maisha yake.
“Tunaomba mkamilishe haraka utaratibu wa malipo ya fidia na yaende sambamba na uhamishaji wa wananchi na mlete hizo taarifa wizarani. Pia tunataka tujue ujenzi wa hizo nyumba unaanza lini na unaisha lini” alisema Dkt. Kiruswa.
Alisema kuwa Rais Samia anatamani kuona utekelezaji wa mradi huo ukiendelea kwa kasi ili kutimiza lengo la kuanzishwa kwake, kwakuwa mgodi huo unazalisha miongoni mwa madini ya kimkakati ambayo kwasasa mahitaji yake ni makubwa duniani.
Aliutaka mgodi huo kupeleka huduma zote muhimu kama shule, barabara na maji, katika maeneo utakaohamishia watu ili wapate huduma zote muhimu kwani ni haki za msingi.
Pia aliwataka kushirikiana na Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini ikiwemo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ili wawe wadau muhimu , tunategemea kuwa mtashirikiana nao ili kubadilishana uzoefu” amesema Dkt. Kiruswa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tembo Nickel, Benedict Busunzu alisema kuwa Mgodi huo umechangia Shilingi Bilioni 18 kupitia kodi na malipo ya leseni.
Pia, aliongeza kuwa kupitia huduma za ugavi zaidi ya Shilingi Bilioni 43 zimetumika ambapo kati ya fedha hizo Wilaya ya Ngara imetumika asilimia 2, sehemu nyingine za Tanzania asilimia 95, kutoka nje ya nchi ni asilimia 3.
Kwa upande mwingine, Afisa anayeshughulikia uhamishaji wa watu na makazi Basil Shio, alieleza kuwa tayari wamewapa waguswa wa mradi mafunzo ya namna bora ya matumizi ya fedha ambazo watalipwa kama fidia.
Aidha, aliongeza kuwa waguswa 349 wa mradi huo wameshaonyeshwa mfano wa nyumba na kuna maeneo 7 yametengwa ambayo watu hao wamechagua wenyewe maeneo wanayopendelea kujengewa nyumba zao na Kampuni.
Naye, Mbunge wa jimbo la Ngara, Mkoani humo, Mhe. Ndaisaba Ruhoro alikiri kuwa wananchi wa Ngara wanafarijika kuona kuwa wenyeji wanapata nafasi za kuajiriwa katika mradi kwani itasaidia familia nyingi kujikwamua kiuchumi.