Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) Bw. Isack N. Kihwili akizungumza na Wahariri wa Vyombo katika semina ya kuwajengea uwezo iliyofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo Septemba 21, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika semina.
………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imesema itaendelea na utaratibu wa kutoa fidia Shilingi 7, 500,000 kwa wateja wa benki ambazo zimefilisiwa jambo ambalo lisaidia kuongeza imani na utulivu kwa wananchi kwenye mfumo wa sekta ya benki katika kuhakikisha amana zao zinakuwa salama.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari leo Septemba 21,2023 jijini Dar es Salaama katika Semina ya kuwajengea uwezo kuhusu Bima ya Amana, Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) Bw. Isack Kihwili, amesema kuwa March, 2023 serikali iliongeza kiwango cha fidia ya amana hadi kufikia Sh. 7,500,000 kwani awali walikuwa wanatoa fidia ya Sh. 1, 500,000.
“Serikali imeamua kuongeza amana ya fidia kutoka Sh. 1, 500,000 hadi Sh, 7,500,000 kutokana na thamani ya fedha, mfuko umekuwa na uwezo wa kutoa kiasi hicho kwa sasa pia imekuwa sikivu baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wananchi” amesema Bw. Kihwili.
Amesema kuwa baadhi ya wateja wa benki ambazo zipo chini ya ufilisi kuna kiwango cha fedha ya bima ya amana Sh. 1,500,000 bado hawajachukua kutokana sababu mbalimbali wanapaswa kwenda kuchukua fedha zao.
Amebainisha kuwa bado wanaendelea na ufilisi wa benki mbalimbali na mpaka sasa wapo katika hatua ya ukusanyaji wa mali za benki ikiwemo mikopo.
“Tayari tumepata kampuni mbili za udalali na hivi karibuni wataaza ufatiliaji wa mikopo, tunaomba wananchi ambao wamekopa watoe ushirikiano kwa madalali, kuna changamoto mtu akikopa benki na hiyo benki ikifilisika anajua jukumu la kulipa limeishia, hiyo ni dhana potofu” amesema Bw. Kihwili.
Hata hivyo ameeleza kuwa lengo la semina ni kuongeza uwelewa wa vyombo vya habari jambo ambalo ni rafiki katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu DIB.
Bw. Kihwili amesema kuwa wahariri wa vyombo vya habari wamepata uwelewa kuhusu bima ya amana ambao ni utaratibu wa serikali imeamua kuanzisha kwa ajili ya kuwalinda wateja wa benki.
“Ni muhimu kuwa na amana ya bima kwa sababu inasaidia kuongeza Imani kwa wananchi kwenye mfumo wa benki na kuongeza utulivu katika sekta ya benki hasa mteja akiwa na uhakika amana yake ipo salama” amesema Bw. Kihwili.
Amesema kuwa bima ya amana ni taasisi ya serikali ambayo imeundwa kisheria ikiwa na jukumu la kutoa bima ya amana kwa ajili ya wateja mbalimbali wa benki.
DIB ni Dhima ya kuhamasisha imani kwa umama katika sekta ya Benki na hivyo kuchangia utulivu wa kifedha kupitia ulinzi wa amana nchini.
Kazi yake ni kusimamia mfuko wa amana, kulipa fidia kwa wenye amana pale ambapo Benki au Taasisi ya fedha inapofilisika, kusimamia ufilisi wa Benki na taasisi ya fedha pale ambapo Bodi ya Bima ya Amana itateuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kufanya kazi yake.
Amana zilizopo katika Benki na taasisi za fedha zina Kinga (BIMA) ya Bodi ya Bima ya Amana kwa mujibu wa Sheria na Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.