Taasisi ya Mwalimu Nyerere Yawataka viongozi Kilimanjaro kujenga Umoja,utulivu na Amani,huku wakimuenzi Mwalimu kwa vitendo.
TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere,imewataka viongozi wa taasisi hiyo Mkoa wa Kilimanjaro wawe mfano wa kuigwa katika kumuenzi Baba wa Taifa la Tanzania,Hayati Julius Nyerere kwa kujenga umoja,utulivu na Amani ya nchi yetu ya Tanzania.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,Paul Kimiti alipotembelea makao Makuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro kwaajili ya kutambulisha uongozi mpya wa Taasisi hiyo Mkoani hapa ambapo ikiwa ni Moja ya muendelezo wa kufungua matawi ya kumuenzi Baba wa Taifa katika kila Mkoa hapa Nchini.
“Tumepata viongozi hapa Kilimanjaro wakiongozwa na Mwenyekiti Alhaji Shayo ambaye amejitolea,wao na sisi hatulipwi hata Senti tano na huu ndio mfano wa kuigwa na Mungu atawabariki katika kulitumikia Taifa hili.”
“Tunataka Kilimanjaro iwe mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine katika kujenga Umoja,utulivu na Amani ya nchi yetu maana hapa ndipo chimbuko lenyewe la kihistoria,wasije wakaudharau mlima Kilimanjaro maana una historia kubwa sana kwa baba wa Taifa” amesema Kimiti
Kimiti ameeleza matumaini yake kuwa baada ya muda mfupi kupitia kuzunguka nchi nzima,kila Mkoa hapa Tanzania patakuwa na tawi la kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambapo mpaka Sasa matawi yasiyopungua 20 yamekwisha funguliwa katika mikoa mbalimbali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mkoa wa Kilimanjaro,Alhaj Shayo amewashukuru Viongozi wa Taasisi hiyo ngazi ya Taifa kwa kuja kuwatembelea ambapo amesema mipango waliyoiweka itamsaidia kijana wa kitanzania wa zama hizi ambaye hakuwahi kupata bahati ya kumuona Baba wa Taifa hili kujua namna Nyerere alivyoanza siasa,alivyokuwa na utendaji wake ulivyogusa mioyo ya wengi hapa Nchini ambapo yote atayajua kupitia tawi hilo lililoanzishwa mjini Moshi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,Anton Mavunde amesema lengo la Taasisi hiyo ni kuwakumbusha watanzania hasa vijana wamkumbuke Baba wa Taifa kwa vitendo kwa kuchukia rushwa,vitendo vibaya na mambo kama hayo ili Tanzania iendelee kuwa nchi ya Amani ambapo Nyerere alipandisha Mwenge juu ya kilele Cha mlima Kilimanjaro akitangaza kuwa nchi hii ni ya Amani.
Ikumbukwe Mwalimu Nyerere ndiye mwasisi wa Mwenge wa uhuru na alipouwasha alisema ” tunawasha Mwenge na kuweka juu ya mlima kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka ya nchi yetu,ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini,upendo pale ambapo Pana chuki,heshima ambapo pamejaa dharau”
“Tunataka tuwarithishe vijana mambo mazuri ambayo baba wa Taifa aliyafanya ili nao kwayo iwe mfano tegemezi kwa siku zijazo watakapochukuwa dhamana ya kuiongoza nchi,kitu ambacho tumekuwa tukiona vijana wakiaminiwa kwa Kupewa nyadhifa mbalimbali lakini wakielewa misingi ya baba wa Taifa aliyotuachia watafanya vizuri zaidi” amesema Mavunde
Aidha Mavunde ameongeza kwa kusema “Uzalendo wa nchi yetu,Moyo wa kujitolea kwa nchi Yao,kufanya kazi kwa bidii haya yalikuwa ni mambo ya Mwalimu Nyerere Ikiwa ni pamoja na kuchukia maovu”