Mkurugenzi wa Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Juvenal Nkonoki akizungumza na vikundi vya wavuvi na wachakataji wa dagaa
Mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ambae pia ni mratibu wa mafunzo hayo Dkt.Bonamax Mbasa akizungumza na wachakataji wa dagaa na wavuvi.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo wakiwa ukumbini.
Mwakilishi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Meja Hassan Mrisho akizungumza na washiriki wa mafunzo.
Na Hellen Mtereko,Tanga
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Juvenal Nkonoki amevihimiza vikundi vya Wavuvi na Wachakataji Dagaa vya Wilayani Pangani Mkoani Tanga kudumisha umoja na ushirikiano kwani huo ndiyo mtaji wa maendeleo.
Prof. Nkonoki aliyasema hayo Jumatatu Septemba 18, 2023 katika hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya siku mbili ya kuvijengea uwezo vyama vya ushirika kwa vikundi 11 vya Wavuvi na Wachakata Dagaa vyenye jumla ya wanachama 218 ambapo kati yao Wanawake 118 na Wanaume 100.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Kijiji cha Sakura Kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga.
“Mkiwa katika umoja tunaimani hata tukiwajengea uwezo mtakuwa na nguvu ya kutoka pale mlipo na kwenda sehemu nyingine kwa vile mtakuwa na uwezo wa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi,tunaamini kwa umoja wenu mafunzo haya yanakwenda kuwa chachu ya mabadiliko kwenu na mnao wawakilisha” alisema Prof. Nkonoki.
Aidha Profesa Nkonoki ameishukuru Serikali ya Japan pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kufadhili mafunzo hayo pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uratibu wa Mafunzo hayo.
Awali mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Hassan Mrisho Kheri akitoa ufafanuzi wa Mafunzo hayo, alisema kuwa mafunzo hayo ni moja kati ya malengo ya mradi wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu Nchini, ambapo Februari 2023 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) alizindua Mwongozo wa kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika Bahari na Maziwa Makuu kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo, Dkt. Bonamax Mbasa ambae ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini amesema mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo yanafanyika katika Wilaya tatu ambazo shughuli zake za kiuchumi zinategemea uvuvi baharini ambazo ni Mafia, Pangani na Bagamoyo.