Mkuu wa wilaya ya Mbulu Komredi Kheri James mapema leo ameshiriki na kukabidhi mchango kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika zoezi la kuichangia Redio habari Njema inayo endelea na zoezi la kukusanya kiwango cha shilingi milioni hamsini ili kuimarisha utendaji wake.
Komredi Kheri James amewasilisha mchango huo kwa Mhashamu Askofu Antony Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu na ametumia fursa hiyo kuwasilisha salamu za Serikali na Dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha uhuru na mazingira ya utendaji wa vyombo vya habari nchini, pamoja na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Taasisi za dini katika kuhudumia jamii katika sekta mbalimbali.
Akizungumza katika zoezi la uchangiaji, Kheri James ameeleza kuwa Redio habari njema ina stahili kuungwa mkono kutokana na kazi kubwa ya uelimishaji,uhabarishaji na juhudi kubwa zakuhamasisha maendeleo na kusimamia maadili.
Kwa upande wake Mhashamu Askofu Antony Lagwen amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuunga mkono juhudi za Jimbo Katoliki la Mbulu na ameshukuru kwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Kanisa na Serikali katika kuwatumikia na kuwahudumia Wananchi.
Redio habari Njema inarusha matangazo yake kutokea wilaya ya Mbulu, na ndio Redio tegemeo kwa wananchi walio wengi wa Wilaya ya Mbulu na maeneo ya jirani.