Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis akipokea zawadi ya picha yake iliyochorwa kutoka kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha Watoto cha Bibi Mimi Girls Home wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kufuatilia utekelezaji wa Sera na Afua mbalimbali za maendeleo na Ustawi wa Jamii Septemba 16, 2023.
Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na wananchi wa Kata ya Sukuma Wilayani Magu mkoani Mwanza wakati wa ziara yake mkoani humo kufuatilia utekelezaji wa Sera na Afua mbalimbali za maendeleo na Ustawi wa Jamii Septemba 16, 2023.
……..
Na WMJJWM Magu-Mwanza
Wananchi wa Kata ya Sukuma Wilayani Magu mkoani Mwanza wamehamasika katika kuboresha makazi yao na kujenga nyumba 165 kwenye Kata 4 za Wilayani humo.
Hayo yamebainika katika ziara ya Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Magu kufuatilia utekelezaji wa Sera na Afua mbalimbali za maendeleo na Ustawi wa Jamii Septemba 16, 2023.
Akitoa taarifa ya Kampeni ya Makazi Bora Wilayani humo Mkurugenzi wa Kivulini Yasin Ali amesema Shirika hilo limefanikiwa kuhamasisha Jamii katika kuboresha makazi yao kwa kutumia vikundi mbalimbali vya umoja ikiwemo Wanawake na mashabiki wa Timu za mpira wa Miguu.
“Mhe. Naibu Waziri tumefanikiwa kuhamasisha wananchi kuachana na nyumba za nyasi na kujenga nyumba za bati na Bora na tumekuja na namna ya kipekee ya kuhamasisha Jamii kwa kuhusisha mashabiki wa Timu za mpira za Simba na Yanga ili waungane pamoja kusaidiana kuboresha makazi yao ” alisema Yasin
Aidha ameongeza kuwa Shirika la Kivulini limehamasisha makazi Bora na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto katika Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Mara, Geita na Shinyanga uwepo wa Kampeni hiyo imesaidia kutoa elimu na kubadilisha fikra ya Jamii kupambana na vitendo vya ukatili na kuboresha makazi yao.
Akizungumza na wananchi Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis amesema Wizara inafanya Kampeni ya Makazi Bora katika Mikoa mbalimbali kwa kushirikiana na Mikoa na Halmashauri ambapo kuanzia Julai 2022 hadi Aprili 2023 jumla ya nyongeza ya nyumba 732 zilijengwa kwa hamasa ya Kampeni hiyo na kufikisha jumla ya nyumba 5712.
Amesema kuwa maendeleo endelevu yanatokana na wananchi wenyewe hivyo ameihamasisha Jamii kuongeza juhudi kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo Kampeni ya Taifa ya ujenzi wa Makazi bora na kukuza Moyo wa uzalendo katika kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo kwa kutumia rasimali zilizopo.
“Katika ziara yangu nimemtembelea nyumba ya Mama aliyenyanyasika na Mumewe na kuachwa na Watoto ila akuwa mnyonge akapambana na sasa ameshaanza kujenga nyumba bora ili watoto wake waishi katika hali nzuri”alieleza Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi amepongeza juhudi za Shirika Lisilo la Kiserikali la Kivulini kwa kuhamasisha Jamii na kutoa elimu ya kupinga ukatili, malezi na Makuzi na kuboresha makazi katika jamii kwenye Mikoa mbalimbali nchini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kasanda amesema kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameshirikiana na Serikali kufanya kazi kubwa ya kuingia kwenye Jamii kwa kutoa elimu katika kuonana changamoto mbalimbali ikiwemo kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na kuboresha makazi katika maeneo yao.
Nao Baadhi ya wananchi wameishukuru Serikali kwa kuunganisha nguvu pamoja na wadau kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na kuhamasisha Jamii katika kuboresha makazi yao.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Makao ya Watoto ya Main Springs kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Magu na amewaasa wamiliki wa Makao ya Watoto nchini kuendesha Makao kwa kuzingatia Sheria, taratibu, mila na desturiza kitanzania.