OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24 shule za msingi 1,000 zitajengwa kwenye kila Mkoa nchi nzima ili kuimarisha ubora wa elimu ya awali na msingi kwa watoto wetu.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akitoa salamu za Wizara yake mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Mtwara na wakati akifanya mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Masasi leo tarehe 17.09.2023.
Amesema ‘ Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali na katika mwaka huu wa fedha tutajenga shule za msingi 1,000 zitazosaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye baadhi ya shule hivyo kuongeza ubora wa Elimu.
Halkadhalika katika Mkoa wa Mtwara Mhe. Mchengerwa amesema Serikali imewatengea shilingi Bil.6.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Elimu ya Msingi na Sekondari.
Akizungumzia Wilaya ya Masasi amesema Wilaya hiyo imepata fedha kupitia Mradi wa Lipa kulingana na matokeo (EP4R) na kupitia Mradi wa SEQUIP kiasi cha shilingi Mil 585 zimeletwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari.
Halkadhalika Mchengerwa amesema kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo ni ya zamani na imechakaa hivyo imetengewa fedha shilingi Bil. 1.2 kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa hospitali hiyo; Na kwenye Miundombinu ya barabara za Lami mtandao utaongezwa kutoka Km 6.9 zilizopo hivi sasa mpaka Km 11.2 za Lami.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yuko katika ziara ya Kikazi mkoani Mtwara na siku ya leo ametembelea na kukagua miradi na kusalimiana na Wananchi katika Halmashauri ya Nanyumbu, Masasi Mji na Masasi Dc.