Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali inatoa ruzuku kwa wakulima ili kuwawezesha zaidi katika shughuli za kilimo sambamba na kusaidia Serikali kupata mapato.
Kauli hiyo ameitoa jana Septemba 16, 2023 katika Wilaya ya Tandahimba, Mkoa wa Mtwara wakati akizungumza na wananchi katika Uwanja wa Majaliwa.
“Tunaleta ruzuku kuwaongezea uwezo wa kuzalisha mazao, tunataka kila shilingi moja ya ruzuku izalishe shilingi tatu hadi tano”, amesema Rais Samia.
Mhe. Rais Samia ameongeza “Nendeni mkafanye kazi kwa kuwa Serikali inaleta ruzuku kwa gharama kubwa ili kuwawezesha wakulima. Wagawaji wa pembejeo najua kuna ujanja na kutoa takwimu za uongo kwa lengo la kuwanyima pembejeo wananchi, viongozi fanyienikazi”.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema mwaka 2023, Serikali itatoa shilingi bilioni 105 katika Mkoa wa Mtwara na hivyo amewataka viongozi kusimamia vizuri sekta ya kilimo mkoani humo.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuwa katika Wilaya hiyo ya Tandahimba wamesajiliwa zaidi ya wakulima 100, na hivyo kuwataka wakulima zaidi waendelee kujisajili.
Kuhusu mikakati ya Serikali ya kuboresha kilimo mkoani humo, Waziri Bashe amesema “Katika bajeti ya mwaka huu katika eneo la umwagiliaji tumetenga fedha kwa ajili ya usanifi wa mabonde ya kina yaliyopo Mtwara”.
Akifafanua zaidi kuhusu skimu mbili za umwagiliaji kati ya nne ambazo Serikali itaboresha amesema ” Skimu ya Lihenje yenye ekari 211 itaboresha mwaka huu, Skimu ya Chiumo yenye ekari 500 inatangazwa. Pia, skimu za umwagiliaji 100 zinafanyiwa upembuzi yakinifu”.
Kuhusu mpango wa Serikali wa kuongeza tija katika zao la korosho, Waziri Bashe amesema mwezi Novemba mwaka 2023 Serikali itaanza kujenga kiwanda cha kubangua korosho mkoani Mtwara.
“Mkulima akianza kubangulia korosho nyumbani maana yake mapinduzi ya korosho yameanza, tukijenga kiwanda Kalanje mkibangulia nyumbani mtauza pale na mtauza pia maganda yake”, amefafanua Waziri Bashe.
Amesisitiza”Niwaombe wenye mikorosho ya zamani anzeni kiiondoa, Naliendele watazalisha miche ya korosho na kuigawa bure”.