Mwandishi wetu, Arusha
Jeshi la polisi Mkoa Arusha, limecharuka kufuata walinzi wa Kampuni ya Mengwe kutajwa kuhusika na tukio la ujambazi na sasa walinzi wote Mkoa Arusha kuhakikiwa.
Walinzi wawili wa kampuni hiyo wanasakwa kuhusika na ujambazi, kwenye makazi ya Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Predators Safari Club LTD, Yusuph Khan eneo la Kiranyi Sakina mkoa Arusha.
Walinzi wa Kampuni hiyo pamoja na watuhumiwa wengine wa wanatuhumiwa kuiba sh 30 milioni na vidani vya dhahabu vyenye thamani ya sh15 milioni, Septemba 10 na kukimbia .
Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Justine Masejo amesema wameanza kuhakikisha wafanyakazi wa kampuni za ulinzi, kwa kuchukuwa alama za vidole na kupata taarifa zao ili kuzihifadhi.
“Tutapita kwenye hizi kampuni na kuchukuwa alama za vidole na taarifa za wafanyakazi kwani watu, wanakodisha hizi kampuni za ulinzi ili walindwe lakini siyo kuibiwa,” amesema kamanda Masejo.
Amesema kutokana na tukio hilo la wizi polisi bado wanaendelea na uchunguzi na tayari wakurugenzi wa kampuni ya Mengwe wamehojiwa na wametakiwa pia kushirikiana na vyombo vya dola kuwakamata watuhumiwa.
“Tumewahoji tayari na wameendelea kutupa ushirikiano ili kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa,” amesema.
Meneja wa Kampuni wa Mengwe Security, Juma Masuka amesema wafanyakazi wawili wa kampuni hiyo, Moses Alfred Mabula (46) na Lazaro Richard Pyuza (37) wanasakwa kwa tuhuma za kushiriki katika ujambazi.
“Bado tunawatafuta hawa walinzi ambao walionekana kwenye kamera za CCTV wakiwa wanawafungulia geti majambazi lakini pia walishiriki kupora kwa kuwaweka chini ya ulinzi Khan na familia yake na baadae kukimbia,” amesema.
Amesema walinzi hao waliokuwa ni wakazi wa eneo la Daraja mbili wamekimbia tangu kufanya ujambazi huo lakini watahakikisha wanakamatwa na akatoa wito wananchi watakao waona kutoa taarifa polisi.
Kampuni ya Predators Safari imetangaza kutoa zawadi ya sh 2 milioni kwa ambao watafanikisha kukamatwa watuhumiwa hao.