Na Joachim Nyambo, Mbeya.
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtanila iliyopo kijiji cha Igangwe wilayani Chunya mkoani Mbeya amefariki dunia baada ya kunywa kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni sumu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga tukio hilo limetokea kijijini Igangwe jana, Septemba 14 mwaka huu saa moja na nusu asubuhi.
Kamanda Kuzaga alimtaja Mwalimu Mkuu huyo kuwa ni Magwira Nkuta(41) mkazi katika kijiji cha Igangwe wilayani Chunya.
Alisema chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo kwani inadaiwa kuwa kabla ya ujio wa mbio za Mwenge wa Uhuru, marehemu alikabidhiwa fedha na ofisi ya Takukuru kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kibao cha “KLABU YA
TAKUKURU RAFIKI SHULENI” lakini pamoja na kutumiwa fedha hizo hakuweza kutengeneza kibao hicho hadi Mwenge wa Uhuru ulipofika shuleni
hapo kwa ajili ya ufunguzi wa Klabu hiyo.