Meneja TRA Mkoa wa Mwanza Ernest Dundee akitambulisha kampeni ya tuwajibike iliyozinduliwa leo.
Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza Ernest Dundee akiendelea kutoa elimu kwa Wafanyabiashara.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza Ernest Dundee akitoa elimu ya kutoa risiti halali za EFD pindi mteja anaponunua bidhaa.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza imezindua rasmi kampeni inayojulikaa kwa jina la ‘Tuwajibike’ yenye lengo la kuwakumbusha na kuwasisitiza wauzaji wa bidhaa na wanunuzi kutoa na kudai risiti halali za EFD.
kampeni hiyo imezinduliwa leo Ijumaa Septemba 15, 2023 katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa kutambulisha kampeni hiyo kwa waandishi wa habari na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo Meneja wa TRA Mkoani hapa Ernest Dundee, amesema kampeni hiyo ni endelevu na inamalengo makuu matatu ikiwemo kuwakumbusha na kuwahamasisha wanunuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali kudai risiti halali za EFD pamoja na kuzikagua ili kubaini kama zina thamani halisi ya kiasi cha fedha kilicholipwa.
” Kwamfanyabiashara risiti ni mwanzo wa kuwa na kumbukumbu na taarifa sahihi za shughuli za biashara anazofanya lakini pia kwa mnunuzi kuwa na risiti halali yenye maelezo na thamani sahihi ya bidhaa ulizonunua inakupa uhalali wa kumiliki bidhaa hizo”, amesema Dundee.
Aidha amesema kampeni hiyo pia imelenga kufuatilia utoaji wa risiti halali za EFD katika maeneo mbalimbali ya biashara pamoja na kuchukua hatua kwa wauzaji wasiofuata sheria katika utoaji wa risiti hizo, sanjari na kuwachukulia hatua za kisheria kwa wafanyabiashara wanaotumia risiti moja wakati wa kusafirisha mizigo pamoja na kuuza risiti pasipokuwa na manunuzi yoyote.
Ameeleza katika kampeni hiyo watumishi wa Mamlaka hiyo watapita katika maeneo mbalimbali ya biashara ili kukagua kama mnunuzi amepewa risiti halali.
Baada ya kampeni hii kaguzi za kawaida za matumizi sahihi za EFD zitaendelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kutekeleza wajibu wa kisheria.
Pemela Kanza na Upendo Mwakyolile ni wafanyabiashara wamesema kunafaida kubwa katika kutoa risiti kwani wakati wa kupewa makadilio ya kodi inakuwa ni rahisi na mpangilio mzima wa mauzo unaonekana hata kama hujaweka kumbukumbu kwenye kitabu.