Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa katika ufunguzi wa Mkutano wa nne wa Kamati Maalum ya Kitaalam, kuhusu Sekta ya Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda ya Bara la Afrika pamoja na Nishati uliofanyika leo tarehe 15 Septemba, 2023 katika Hoteli ya Golden Tulip Visiwani Zanzibar.
……
Na Grace Semfuko – MAELEZO na Dorina Makaya -Wizara ya Nishati.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono Ajenda ya Maendeleo ya Mwaka 2063 iliyowekwa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika- AU ambayo ina mikakati ya kufikia Afrika yenye ustawi na umoja.
Dkt. Biteko ameyasema hao leo Septemba 15, 2023 wakati alipomwakilisha Rais wa Zanzibar Dkt. Husein Mwinyi kufungua Mkutano wa nne wa Kamati Maalum ya Kitaalam, kuhusu Sekta ya Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda ya Bara la Afrika pamoja na Nishati ambapo ameongeza kuwa, jiografia ya Bara hilo ni ya kimkakati na inaturuhusu kuunganishwa na ulimwengu kwa njia ya anga, usafiri wa barabarani na majini na hivyo kuna kila sababu ya Afrika kuendelea kuwa katika umoja huo.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono ajenda ya mtangamano wa Afrika iliyowekwa na AU, ajenda ya 2063 inatupa Dira ya Afrika tunayoitaka ili kufikia Afrika yenye ustawi na umoja, utekelezaji wa mikakati ya ajenda hiyo ni nyenzo muhimu sana ya kutufanya tuyafikie malengo yetu hivyo majadiliano yenu ambayo yanaongozwa na kaulimbiu ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu ili kufikia malengo ya 2063 ni muhimu sana kwenye mkutano huu” amesema Dkt. Biteko
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt Khalid Salum amesema mkutano huo ni fursa nyingine ya kupokea taarifa kuhusu maendeleo yaliyopatikana tangu mkutano uliopita uliofanyika kwa njia ya mtandao mwezi juni mwaka 2021 ambapo kwa sasa, pamoja na mambo mengine, watajadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia malengo ya Bara la Afrika.
”Ninatambua kwamba uwepo wenu kwenye mkutano huu ni ishara yetu ya pamoja ya kuendeleza miundombinu na kupata suluhisho la changamoto za nishati na miundombinu Barani Afrika”* amesema Dkt. Khalid.
Kwa upande wake Kamishna wa Miundombinu kutoka katika Kamisheni ya Umoja wa Nchi za Afrika-AU Dkt. Amani Abou-Zeid amesema Afrika haina budi kuharakisha maendeleo ya miundombinu ili kuleta ushindani na katika ushiriki wa watu wa Bara hilo katika soko la kimataifa la bidhaa.
“Kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya Afrika ni jambo la kipaumbele, haijalishi kuwa miundombinu yetu ni mizuri kiasi gani, sote tunajua kuwa tunahitaji kuharakisha ujenzi wa miundombinu yetu ili kuwe na matarajio makubwa kwa watu wetu, hii ni kwa ajili ya kuleta ushindani katika ushiriki wetu kwenye soko la kimataifa” amesema Dkt Amani.