KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu nchini, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umekabidhi msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 12 kwa shule za Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Akizungumza jana Septemba 13, 2023 wakati wa kukabidhi madawati hayo mbele ya viongozi wa Chama na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo, Mhifadhi Mkuu TFS Shaabani Kiullah alisema Wakala huo kupitia program ya ujirani mwema unaowajibu wa kushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto ndani ya jamii.
“TFS pamoja na shughuli zetu za usimamizi wa misitu na rasilimali zitokanazo na misitu, tumekuwa tukihakikisha rasilimali hizo zinachangia mahitaji muhimu ya jamii, hiki tulichokifanya wilayani hapa ni sehemu ya utekelezaji wa program ya ujirani mwema ambayo tumekuwa tukikifanya na katika maeneo mengine,” anasema Mhifadhi Mkuu huyo.
Akizungumza mara baada ya kupokea madawati hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dustan Kyoba ameshukuru kupatikana kwa madawati hayo na kuahidi kuyagawa kwa wakurugenzi wake ili waweze kuyagawa kwenye shule zenye uhitaji.
“Naipongeza TFS kwa kazi kubwa inayofanya chini ya uongozi wake Prof. Dos Santos Silayo, matunda ya uhifadhi tunayaona, sasa niwaombe wakazi wa Wilaya ya Kilombero kuhakikisha mnashiriki kikamilifu katika kuhifadhi rasilimali misitu na kuacha kabisa kufanya shughuli za kibinadamu sehemu za misitu iliyohifadhiwa” anasema Mkuu wa Wilaya huyo.