Wabunge wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti wakitembelea maabara ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC ) kanda ya kaskazini Njiro.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ,Daniel Sillo akizungumza wakati alipotembelea Tume hiyo jijini Arusha.
…………………………
Julieth Laizer,Arusha .
Arusha .Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Kanda ya kaskazini imekuwa na ongezeko kubwa la maduhuli kwa asilimia 260 ambapo kwa mwaka 2014/2015 walikuwa na uwezo wa kukusanya shs bilioni 2 na kufikia shs 10.6 bilioni kwa mwaka wa fedha uliopita.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ,Profesa Lazaro Busagala wakati akitoa maelezo kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti walipotembelea Tume hiyo.
Profesa Busagala amesema kuwa,wamefanikiwa kukusanya kiwango hicho kutokana na usimamizi mzuri uliosaidia sana kupunguza upotevu wa mapato.
“Fedha hizi zimeweza kutumika katika ununuzi wa mitambo, kujengea maabara,ambapo tulikuwa hatuna maabara Zanzibar ila kwa sasa hivi imeshakamilika kwa asilimia 100,huku kwa jijini Dar es Salaam maabara ikikamilika kwa asilimia 70 ,na upande wa kituo cha kuhifadhi bidhaa mbalimbali ukiendelea .”amesema Profesa Busagala.
Aidha amesema kuwa, hivi sasa wana maabara jijini Mwanza na Dodoma na tayari imeshakamilika kwa asilimia 100 huku ujenzi ukiendelea mkoani Mbeya na lengo kubwa ni kuhakikisha kanda zote zinakuwa na maabara na hii yote ni kutokana na ongezeko la maduhuli.
“Kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo na nchi mbalimbali tumeweza kupata vifaa vyenye thamani ya shs 7 bilioni kutoka Umoja wa Ulaya ambapo tuliweza kuandika andiko na walipoona tumeanza ujenzi ndipo walipotuletea vifaa hivyo.”amesema Profesa Busagala.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo,Daniel Sillo amesema kuwa, wametembelea Tume hiyo kuweza kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali unaofanywa na Tume na wameridhika na matumizi ya fedha zilizotumika katika Tume hiyo katika ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa huku akiipongeza serikali kwa kazi kubwa waliyoifanya katika Tume hiyo.
Sillo ameishauri serikali kuongeza bidii katika swala la kibajeti ili kuongeza rasilimali watu ,vifaa pamoja na fedha kwa ajili ya kuendesha Tume hiyo.
Nao baadhi ya wabunge wakizungumzia kuhusiana na Tume hiyo,Mbunge wa Musoma mjini Vedastus Mathayo wamesema wameridhika na matumizi ya fedha katika miradi mbalimbali na kuwa wanaiomba serikali kuendelea kuongeza bajeti zaidi kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali pamoja na kuendeleza miradi mbalimbali katika Tume hiyo.