……….
Na Prisca Libaga Maelezo
Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania(TFS) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) zimepongezwa kwa kufanya jitahada katika kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinafanyika kwa tija na ufanisi katika maeneo yao.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula alipofanya ziara ya kukagua shughuli zinazofanywa na taasisi hizo katika Pori la akiba la Selous pamoja na shughuli za uhifadhi wa misitu katika wilaya ya Liwale mkoani Lindi
Aidha, Mhe. Kitandula akiwa katika kambi ya Miguruwe iliyopo katika pori la akiba Selous alikagua chumba maalumu cha kuangalia hali ya pori ikiwa kuna wanyama waliotoka kwenye maeneo hayo ya asili au hali ya matishio ya moto katika pori hilo.
Mhe. Kitandula alitumia fursa hiyo kuwapongeza TAWA kwa kuwa na mfumo huo wa kuhakikisha wanyama waharibifu wanadhibitiwa ipasavyo ili kuepusha migogano kati ya binadamu wanaishi pembezoni mwa maeneo hayo na wanyama wakali na waharibifu.
Sambamba na hayo, Mhe. Kitandula amewapongeza TAWA kwa kuamua kuanzisha karakana ya kisasa kwa ajili ya kutengeneza magari yanayofanya doria kwani kwa kufanya hivyo itapunguza gharama na kusaidia dori zifanyike kwa ufanisi.
Aliongeza kuwa uhifadhi unahitaji kufanya kazi kwa tija na kwa haraka lakini pia umakini katika kutekeleza majukumu hayo, hivyo kuwa na karakana na mfumo wa kuangalia hali ya pori ilivyo italeta matokeo chanya katika shughuli nzima ya uhifadhi maliasili katika ukanda wa Kusini.
Kwa upande wa Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ya Wilayani Liwale, Mhe. Kitandula aliwapongeza kwa kazi nzuri ya uhifadhi na kuwasisitiza waendelee kuchapa kazi.
Awali akitoa taarifa ya wilaya Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Mhe. Goodluck Mlinga alimpongeza Mhe. Naibu Waziri kwa kuteuliwa na kuaminiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumuomba washirikiane kutatua migogoro mbalimbali iliyopo katika eneo hilo inayosababishwa na muingiliano kati ya binadamu na wanyama wakali na waharibifu
Akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ya Wilayani Liwale, Afisa Mhifadhi daraja la kwanza Gaudence Francis alisema kwamba wataendelea kushirikiana na mamlaka za wilaya katika kuandaa na kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji vinavyopakana na hifadhi za misitu ili kuondoa mingiliiano ya mipaka na matumizi ya ardhi baina ya vijiji na hifadhi.