Na Beatrice Sanga-MAELEZO
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kimesema kitahakikisha kinaongeza wigo wa utoaji huduma kwa kujenga, kuimarisha pamoja na kuboresha miundombinu yake ili kuwa kituvo cha Uchumi wa Mikutano na utalii barani Afrika pamoja na kuongeza wateja wake wa ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa Septemba 14, 2023 na Ephraim Mafuru Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho wakati akiwasilisha ripoti ya mafanikio ya AICC kutoka mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023 katika Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, na wahariri wa Vyombo vya habari kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ambapo amesema miongoni mwa mabadiliko wanayotarajiwa kuyafanya ni pamoja na kuboresha Ukumbi mbalimbali wa Mikutano, huduma za malazi, usafiri, maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de Change), migahawa na huduma za matibabu (Medical services).
Mafuru amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2019 Kituo hicho kilikumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo mlipuko wa Uviko-19, jambo lililochangia kukosekana kwa huduma na kupungua kwa shughuli mbalimbali ikiwemo uchumi wa mikutano ya kimataifa pamoja na watalii, hata hivyo utendaji kazi wake kutoka 2021/2022 umeimarika na hivyo kusababisha kupandisha mapato yake.
“Utendaji kazi wetu kwa miaka iliyopita haukuwa mzuri sana, tumekuwa tukijiendesha kwa hasara, kulikuwa na uchakavu wa miundombinu yetu lakini pia wageni walikimbia, COVID-19 ikapiga, kwakweli uchumi wa mikutano uliyumba dunia nzima, tumekuwa tukijiendesha kwa mapato ya chini, lakini baada ya mapato yetu kushuka yameanza sasa kuongeza, tulikuwa na mapato ya bilioni 11 tukaenda bilioni 14 lakini tumeenda hadi bilioni 18 kwa hesabu zilizoishia mwezi juni mwaka huu.” Amefafanua Mafuru.
Mafuru amesema pamoja na changamoto walizopitia na ambazo zinaendelea kuwakumba kama vile kuchakaa kwa miundombinu na vifaa, madeni na ukosefu wa rasilimali fedha kwaajili ya kuendesha vituo hivyo kwa ufanisi lakini kwa sasa hali ya uchumi wa mikutano imeanza kuimarika hivyo kuimarisha miundombinu kutasaidia zaidi kuvutia watu na kampuni mbalimbali kufanya shughuli za uchumi wa mikutano na utalii ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
“Vituo vya mikutano ndo vinachangia kwa asilimia kubwa ikifuatiwa na hospitali, AICC imeleta zaidi ya bilioni 5.4 na JINCC imeleta zaidi ya bilioni 4.4 lakini tuna hospital ambayo imeleta zaidi ya bilioni 4.5 ambazo kwa sasa zimeanza kupanda na tunaamini tutazipandisha zaidi, ni kweli tumejiendesha kwa hasara kwa miaka kadhaa lakini kuanzia 2021/2022 tumeendelea kujiendesha kwa faida, mwaka 2022 tumejiandaa kwa faida kutoka kwenye hasara ya milioni 500 kwenda kwenye faida ya bilioni 1.1” ameeleza Mafuru.
Mkurugenzi huyo amewaomba viongozi wa Taasisi za serikali na wadau mbalimbali wanaodaiwa na Kituo hicho wahakikishe wanalipa madeni ili kurahisisha utendaji kazi wenye ufanisi na uboreshaji wa miundombinu ya Kituo hicho.
“Tuna shida kubwa ya watu kutokulipa madeni, mpaka tunaandaa ripoti hii AICC NA JINCC ilikuwa inadai Taasisi zote na wateja bilioni 7.4 na bahati mbaya kati ya Taasisi 20 zinazodaiwa, 17 ni za serikali, tumeomba msaada kwamba hizi Taasisi zinazodaiwa zilipe madeni, niwaombe wakuu wa Taasisi mlipe madeni ili Taasisi zetu ziweze kujiendesha kwa faida.” Amesisitiza Mafuru.
Kwa sasa Kituo hicho kimejipanga kuimarisha utendaji kazi kwa kuanzisha utaratibu wa kupima utendaji kazi wa wafanyakazi wake, kuimarisha mitandao yake ya Kijamii ikiwemo Tovuti yake, kuongeza ushirikiano na wadau mbalimbali kama vile Bodi ya Utalii (TTB) Mashirika ya Ndege ya ndani nan je ya nchi, Ubalozi mbalimbali wa Tanzania nje ya nchi, kujenga Kituo cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC).