Mwenyekiti wa Waendesha Baiskeli Klabu ya TWENDE BUTIAMA, Bw. Butiama Gabriel Landa (wapili kushoto) akimkabidhi namba ya kuchangia ziara ya kwenda Butiama Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Bi. Zuweina Farah (wapili kulia) leo Septemba 13, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Bi. Zuweina Farah akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 13, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waendesha Baiskeli Klabu ya TWENDE BUTIAMA, Bw. Butiama Gabriel Landa akionesha namba ya kuchangia ziara ya kwenda Butiama kwa ajili ya kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Waendesha Baiskeli Klabu ya TWENDE BUTIAMA wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Bi. Zuweina Farah.
………
Taasisi Vodacom Tanzania Foundation imetoa zaidi ya shilingi milioni 250 kwa ajili ya kudhamini Waendesha Baiskeli kwa ajili ziara ya kwenda Butiama ikiwa na lengo la kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na kukuza utalii wa ndani, kuhamasisha utuzaji wa mazingira, elimu na afya jambo ambalo linakwenda kuleta tija kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Bi. Zuweina Farah amesema kuwa waendesha Baiskeli wa Klabu ya TWENDE BUTIAMA kila mwaka wanafanya ziara ya kwenda Butiama wakitokea Dar es Salaam kwa ajili ya kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Amesema kuwa zaidi ya miaka mitano klabu ya Waendesha Baiskel TWENDE BUTIAMA imekuwa ikifanya kazi ya vizuri pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa shughuli za ukuaji wa uchumi kwa maendeleo ya Taifa katika nyanja mbalimbali.
“Tunajivunia kuungana nao Jumuiya ya Waendesha Baiskel TWENDE BUTIAMA kama washirika katika kufanikisha zoezi hili muhimu” amesema Bi. Farah.
Amesema kuwa Vodacom Tanzania Foundation ni taasisi ndani ya Kampuni ya Mawasiliano Vodacom Tanzania ambapo inafanya kazi ya kuisaidia jamii hivyo wanajivunia kuwa wadhamini ya ziara ya kwenda Butiama.
Amesema kuwa “Tunashirikiana na ‘Afya Checkers’ ambao ni wataalamu wa huduma ya afya kuandaa kambi ya kutoa Huduma ya Matibabu ya bure katika mikoa ya Mwanza, Bunda, na Butiama ikiwa ni juhudi zetu za kupambana na magonjwa ya kuambukiza nchini Tanzania vilevile kuchangia vifaatiba kwa Hospitali ya Wilaya ya Butiama,”
Mwenyekiti wa Waendesha Baiskel Klabu ya TWENDE BUTIAMA, Bw. Gabriel Landa ameishukuru Vodacom Tanzania Foundation kwa kutoa msaada ambao utawasaidia kufikia Shule nyingi na kuboresha vifaa tiba, huku akibainisha kuwa msafara wa Waendesha Baiskeli unatarajia kuondoka Jijini Dar es Salaam Oktoba 1, 2023 na kuwasili Butiama Oktoba 14.
Amesema kuwa wameamua kutumia baiskeli katika msafara kwa sababu Nyerere alikuwa anatumia baiskeli katika shughuli zake.
Amesema msafara huo wa baiskeli unashirikisha Watanzania kutoka maeneo mbalimbali wanawaendesha baiskeli.
Urithi wa tukio la Twende Butiama kwa miaka mitano sasa limekuwa likiangazia masuala yanayogusa mazingira kwa kufanikisha kampeni ya upandaji miti.
Kwa kuongezea, jitihada za kuchangisha fedha kupitia kampeni ya “Changia Dawati, Tokomeza Ujinga” zinaonyesha kujizatiti katika elimu, kuwezesha usambazaji wa madawati takribani 200 katika shule za msingi 6 kwa mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, na Mara.