Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Tunduru,wakifuatilia hafla ya utiaji saini mikataba minne ya maji yenye thamani ya Sh.bilioni 5.4.
Meneja wa Ruwasa wilayani Tunduru Mhandisi Maua Mgallah akitoa taarifa ya huduma ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini kabla ya kusainiwa kwa mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji wilayani humo.
Katibu Tawala wa wilaya ya Tunduru Milongo Sana akizungumza kabla ya utiliaji saini wa mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji kati ya Ruwasa na Wakandarasi yenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 5.4 inayokwenda kutekelezwa katika vijiji mbalimbali wilayani humo.
Meneja wa Ruwasa wilayani Tunduru Mhandisi Maua Mgallah kushoto na mwakilishi wa wakandarasi waliopewa kazi ya ujenzi wa miradi ya maji ambaye hakufahamika jina mara moja ,wakitiliana saini ya mikataba ya ujenzi wa miradi hafla iliyofanyika katika Ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa wilaya Tunduru.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro kushoto akikabidhi mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji wa Misechela-Liwanga wenye thamani ya Sh.bilioni 3,020,150,910.00 kwa mkandarasi wa mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Wakili Julius Mtatiro wa nne kulia, akiwa katika picha ya pamoja na wakandarasi,
wahandisi wa Ruwasa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa miradi minne ya maji wilayani humo, wa kwanza kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando,wa pili kushoto mwakilishi wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Bathlomeo Matwiga,wa tatu kushoto Meneja wa Ruwasa Mhandisi Maua Mgallah,Katibu Tawala wa wilaya Milongo Sanga na wa tatu kulia Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo Abdala Mtila.
……
Na Muhidin Amri, Tunduru.
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imetiliana saini na wakandarasi mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya Sh.bilioni 5,473,744,522.32.
Miradi hiyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 70.2 hadi kufikia asilimia 85 kwa wananchi waishio vijijini ifikapo mwaka 2025.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Maua Mgallah,ameitaja miradi hiyo ni mradi wa maji Misechela-Liwanga wenye thamani ya Sh.bilioni 3,020,150,910.00,mradi wa maji Tuwemacho wenye thamani ya Sh.bilioni 1,054,232,603.55 mradi wa maji Msinji utakaotekelezwa kwa Sh.bilioni 1,069,014,450.00 na mradi wa Hulia uliotengewa Sh. Sh.bilioni 1,206,605,519.28.
Aidha alisema,Ruwasa inatarajia kutekeleza miradi miwili ya Namwinyu-Namakunga wenye thamani ya Sh.milioni 450,000,000 na mradi wa Nakapanya-Namakambale kwa gharama ya Sh. 150,000,000 hivyo kufanya miradi itakayotekelezwa kwa mwaka 2023/2024 kufikia 9 kwa gharama ya Sh.bilioni 6,950,003,482.83.
Mgallah alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Ruwasa ilitengewa jumla ya Sh.bilioni 3,890,260,834.14 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitano inayoendelea kujengwa pamoja na uchimbaji wa visima.
Alisema,kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa watu 43,625 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.6 ya wakazi wa vijijini,hivyo kufikia asilimia 82.6. ya utoaji wa huduma ya maji.
Pia alieleza kuwa,katika utekelezaji wa miradi ya maji kupitia wafadhili kwa mwaka 2022/2023 Kanisa la Angliana Doyasisi ya Masasi ilijenga miradi ya maji ya bomba katika vijiji vinne vya Lukala,Mindu,Tulingane na Mitwana ambayo imekamilika na inatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 10,232.
Amelishukuru Kanisa la Anglikana ,kuendelea kushirikiana na Ruwasa katika usimamizi na uendelevu wa miradi ya maji katika vijiji hivyo ambayo imewezesha kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 3.04.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro alisema,lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanaoishi vijijini nao wanapata huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 85 na kuwapunguzia kama siyo kumaliza kabisa changamoto ya kwenda umbali mrefukutafuta huduma ya maji.
Mtatiro,ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali wilayani humo.
Amempongeza meneja wa Ruwasa Maua Mgallah na wasaidizi wake,kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ya maji ambayo imepunguza kero ya huduma ya maji hivyo kuwezesha wananchi hasa wanaoishi vijijini kupata muda mwingi kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo,amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo madiwani kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa miradi ya maji na kuwa walinzi wa miradi hiyo badala ya kuwa sehemu ya walalamikaji.
Amewaagiza wakandarasi waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi hiyo,kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili miradi iweze kudumu kwa muda mrefu na kusisitiza kuwa,serikali haitakuwa tayari kupokea mradi wa ovyo uliojengwa chini ya kiwango.
Mwenyekiti wa kijiji cha Tuwemacho Mahamudu Said alisema,wananchi wa kijiji hicho wana matumaini makubwa na serikali yao kwa kuwapelekea mradi mkubwa wa maji ambao unakwenda kuwaondolea adha ya kukosa huduma yam aji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu.