Na Sophia Kingimali
VIONGOZI wa vyama vya Siasa nchini na wadau wa demokrasia wameaswa kuwa waazalendo na kuweka maslahi ya Taifa mbele ili kuilinda amani ya nchi na kuendeleza umoja na mshikamano.
Akizungumza Leo Septembea 13 wakati akifunga mkutano maalum wa Baraza la vyama vya siasa na wadau wa demokrasia makamu wa pili wa rais wa serikali ya mapinduzi Zanzibar Hemed Suleiman Abdula amesema viongozi wa kisiasa wanajukumu la kuhakikisha wanalinda misingi ya amani na demokrasia nchini ambayo ni tunu ya Taifa.
“Katika kudhihirisha azma ya Serikali Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amezielekeza taasisi za Serikali zilizotajwa katika mapendekezo ya kikosi kazi kufanya mazingatio na utekelezaji wa maoni yaliyotolewa na wadau wa demokrasia na viongozi wa vyama vya Siasa”,amesema
Amesema wamepokea mapendekezo hayo na kuyachukua na kwenda kuyafanyia kazi na Yale yote yaliyohusiana na masuala ya sheria yatapewa mazingatio ili kuhakikisha hatua zinachukuliwa na utekelezaji wake utafanywa kwa urahisi
Amesema hali ya Siasa Hadi Sasa ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao katika hali ya amani ambapo Serikali ya Tanzania na Zanzibar zitaendelea kusimamia amani kwa lengo la kuwaletea Maendeleo watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Amesema jukumu la kulinda amani nchini ni jukumu la watu wote hivyo kama viongozi wa kisiasa ni vyema kuelekeza wajibu wao na kuepuka kufanya matendo yanayoweza kusababisha kupotea kwa amani.
Amesema viongozi wa vyama vya Siasa wanajukumu la kulinda amani ya nchi na kujitahidi kwa nafasi zao na kuwasihi wapenzi na wanachama wao kuwa amani iliyopo ni tunu adhimu hawana budi kuilinda kwa namna yeyote.
Aidha amewakumbusha kuishi kwa kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu za nchi hasa katika nyakati za kuendesha mikutano ya hadhara.
Amesema lugha zinazotumiwa na baadhi ya Viongozi wa kisiasa katika kuendesha mikutano sio nzuri na zinaweza kusababisha mpasuko katika nchi .
“Tusipokuwa makini na jambo hili linaweza kusababisha uvunjifu wa amani,nawasihi sana tulinde amani ya nchi yetu kwa maslahi mapana ya Taifa letu”. amesema
Aidha amewata viongozi na wadau wa demokrasia watumie mkutano huo kubadili tabia zao pale ambapo wanaona tabia hizo zinaweza kuvunja amani na mshikamano .
“Wekeni uzalendo mbele kwa Taifa letu kuliko kitu kingine chochote Tanzania yote,mahala popote tunawajibu kuisaidia Tanzania katika kudumisha amani bila madhara yeyote kwani vijana wetu na vizazi vinavyokuja wanatarajia maandalizi mazuri hivyo tunapaswa kuhakikisha amani inaendelea.”amesema
Nae Mwanasiasa mkongwe nchini Steven Wasira amewataka wanasiasa kuheshimiana kwa lengo la kutengeneza umoja na ushirikiano.
Vilevile ,amewataka viongozi wa dini kuendelea kutoa mafundisho ya kiroho kwa waumini wao lakini si kuwafundisha mambo ya kisasa
“Nchi haiwezi kuwa na umoja ikiwa wanasiasa wake wanafanya shughuli zao kwa kutumia uongo ambao hauleti tija kwa Taifa”,amesema Wasira
Wasira amesema siasa ni mfumo wa maisha hivyo haitakiwi kusema uwongo kwa sababu unaweza ukasambalatisha Taifa kwani kila kitu kitafanyika .
Naye, mwanasiasa mkongwe John Cheyo amesema kunatakiwa kuundwa kamati ya rasimu ya katiba kwa sababu tume ya Jaji Warioba tayari imeshazunguka nchi nzima kukusanya maoni na kutoa elimu kwa wananchi hivyo hakuna haja tena ya kuharibu fedha zingine kwa lengo la kukusanya maoni mengine.
Akitolea mfano visiwani Zanzibar amesema hadi leo hii wanakatiba nzuri yenye misingi na amani bila ya kutoa elimu yeyote kwa wananchi.
Nae Mwenyekiti Mstaafu wa jukwaa la katiba(JUKATA) Deus Kibamba amesema siasa za katiba sio Siasa za mashindano ni maridhiano.
Amesema katiba mpya ni ujenzi wa Taifa jipya hivyo mchakato wa katiba ni wa watu wote na si wanasiasa pekee Bali ni watanzania ambao ndio wadau wakuu.
“Hatuwezi kwenda mbele bila kusema tulikwama vipi kwenye mchakato wa mwaka 2014 kwa sababu kulikuwa na michakato mikubwa miwili ya Kitaifa lazima mmoja ufe na mwingine uendelee”,amesema Kibamba.
Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es salaam Kwa siku tatu umekuja na mapendekezo 15 ikiwemo uchanguzi wa serikali ya mtaa kusimimwa na tume ya uchanguzi na si tamisemi ambapo serikali imeahidi kuyashughulikia mapendekezo yote.