Msajili wa Bodi ya Usajili Wahandisi Tanzania (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Wahandisi yanayotarajia kuanza Septemba 13,2023 katika Ukumbi wa Mlimani City.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Mhandisi Benedict Mukama akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Wahandisi yanayotarajia kuanza Septemba 13,2023 katika Ukumbi wa Mlimani City.
Msajili Msaidizi Uendelezaji wa Taaluma Mhandisi Veronica Ninaluro (kushoto) akiwa na Msajili wa Bodi ya Usajili Wahandisi Tanzania (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Wahandisi yanayotarajia kuanza Septemba 13, 2023 katika Ukumbi wa Mlimani City.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anatarajia kufungua Maadhimisho ya 20 ya Wahandisi yanayotarajia kuanza Septemba 13 hadi 15 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yatafanyika kwa muda wa siku tatu ambapo zaidi ya Wahandisi 4,000 kutoka ndani ya nje ya Nchi wanatarajia kushiriki na kupata fursa ya kuonesha kazi zao na kujadili mada mbalimbali za kitaalamu zenye lengo la kuleta tija kwa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12, 2023, Msajili wa Bodi ya Usajili Wahandisi Tanzania (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe, amesema kuwa Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa anatarajia kufungua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Wahandisi Septemba 14, 2023 huku akieleza kuwa ni fursa kwao kwa ajili ya kuongeza wigo katika kufikia malengo.
Mhandisi Kavishe amesema kuwa katika maadhimisho ya wiki ya wahandisi watapokea mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.
Amesema kuwa Wahandisi watapata fursa ya kujadili pamoja na viongozi wa Wizara na Taifa katika kutoa muongozo hasa nini wanapaswa kufanya ili waendelee kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
“Pia tutawatambulisha wahandisi wapya pamoja na kula kiapo kwa ajili ya kufanya kazi kwa uzalendo kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na sio yao binafsi pamoja na kushiriki zoezi la kuchangia damu salama” amesema Mhandisi Kavishe.
Ameeleza kuwa washiriki watapata fursa ya kushiriki mada mbalimbali za kitaaluma ambazo zimelenga ushiriki katika ujenzi wa Taifa pamoja na ushirikishwaji wa rasilimali za ndani (Local Content) na kuzingatia uweledi na kasi ya mabadiliko (Skill Menegment).
“Wakati umefika wa kuwandaa watu wetu kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ambayo inatekelezwa hapa nchini” amesema amesema Mhandisi Kavishe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Mhandisi Benedict Mukama, amesema kuwa mpaka sasa maandalizi yamekamilika, huku akieleza kuwa Wahandisi wataonesha teknolojia za ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhandisi Mukama amesema kuwa Wahandisi wengine kutoka mataifa mbalimbali Duniani watashiriki kwa njia ya mtandao.
“Viongozi wengi wa Kitaifa watashiriki wakiwamo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, wabunge, huu ni mkutano pekee unaofanywa na Wahandisi mara moja kwa mwaka” amesema Mhandisi Mukama.
Amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwa Wahandisi kwa sababu unawaweka pamoja kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kwa ajili ya kufika malengo tarajiwa.
Tangu mwaka 2003 Wahandisi wamekuwa na utamaduni wa kuwa na Wiki ya Wahandisi kwa ajili kuonesha kazi pamoja na kujadili mada zenye lengo la ujenzi wa Taifa.