Mkurugenzi Joasamwe Investment Kapocha Makongoro akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza Soltepu.
Katibu tawala Manispaa ya Ilemela Mariam Msengi akizungumza baada ya uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza Soltepu.
………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wawekezaji wazawa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuanzisha miradi ya aina mbalimbali ili taifa liweze kuwa na mapinduzi ya viwanda kutokana na serikali ya awamu ya sita kuweka mazingira rafiki kwa sekta hiyo.
Wito huo umetokewa jana Jijini Mwanza kwenye uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza Soltepu cha Joasamwe ambacho kimeanza uzalishaji wa bidhaa hiyo ya kufungia bidhaa na matumizi kwenye steshenari.
Katibu Tawala wa Manispaa ya Ilemela Mariam Msengi alisema serikali inathamini juhudi zinazofanywa na wazawa kuitikia wito wa mpango wa maendeleo wa uchumi shindani na maendeleo ya viwanda.
“Serikali iko pamoja nanyi kuwasikiliza ili muweze kupata mafanikio kwenye kazi zenu mnazoanzisha hivyo changamoto ambazo zinawatatiza zinaendelea kuondolewa”alisema Msengi.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi katika Manispaa ya Ilemela Hassan Milanga alisema chama hicho kinapongeza mwitikio wa wazawa kuanzisha shughuli za uwekezaji ambazo zinatoa ajira kwa watanzania.
Alisema ni sera ya CCM kuona kuwa uwekezaji unaendelea kupata msukumo kutoka kwa watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Joasamwe Investment Kapocha Makongoro, alisema kuwa baada ya kubaini kuwa kulikuwa na changamoto ya uwepo wa kiwanda cha Soltepu aliepata msukumo wa kuwekeza kwa kuanzisha kiwanda hicho.
Alisema anaipongeza serikali kwa kushusha kiwango cha fedha za uwekezaji kutoka dola 100,000 na kuwa 50,000 kwa wazawa na vilevile kupewa misamaha ya kuingiza mashine huku akisamehewa kulipa Kodi kwa mwaka mzima.
Meneja wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mwanza Bakari Songwe alisema jukumu la kusimamia ukuaji wa viwanda wanaendelea kulifanya kwa kutoa msaada wa kiufundi ili wawekezaji wafikie malengo.