Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Hassan Khatib Hassan akifungua mafunzo ya siku mbili kwa maafisa Habari na Mawasiliano kwa ya kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi {kushoto} Naibu katibu Mtendaji Idara ya Mipango Tume ya Taifa ya UNESCO Aboud Idd. Khamis na Mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa Zanzibar {SUZA} Imane Duwe Othman huko katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa Zanzibar {SUZA} Imane Duwe Othman akitoa Mafunzo kwa Maafisa Habari na Mawasiliano kuhusu jinsi ya kwenda sambamba na Maendeleo ya Teknologia iliyopo katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo.
Baadhi ya Maafisa Habari , Mawasiliano na Uhusiano wakisikiliza kwa makini Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo.
………
MAAFISA wa Habari, Mawasiliano na Uhusiano nchini wametakiwa kuwa wabunifu katika utendaji wa kazi zao ili kwenda sambamba na ukuwaji wa maendeleo ya teknolojia .
Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo Hassan Khatib Hassan ameyasema hayo katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya waandishi na Maafisa wa Habari wa SMZ kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab.
Amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza wigo mpana wa kupata taarifa nyingi na kwa haraka, hivyo ipohaja kwa maafisa hao kuwa wabunifu katika mawasiliano yao na umma ili maudhui yao yaweze kueleweka kwa urahisi na kuwavutia watu .
Alifahamisha kuwa Maafisa wa Habari wanapaswa kufahamu kwamba wanaishi katika Ulimwengu wa habari feki licha ya kwamba kuna mabadiliko makubwa ya ukuwaji wa sayansi na teknolojia ya kupata habari kwa haraka.
Mkurugenzi huyo alisema kundi hilo linapaswa kuwa makini na kuhakikisha kuwa wanatoa habari sahihi na za kuaminika ili kuepusha upotoshwaji.
Mbali na hayo aliwataka maafisa hao kuwa na mkakati maalum wa kukabiliana na changamoto na matukio yanayotarajiwa katika taasisi zao ili kutoa maelezo ya haraka pale inajitokezea hali ya taharuki katika taasisi hizo.
“Uadilifu na uaminifu katika kazi zenu ni jambo la lazima hivyo mnapaswa kuwa waadilifu ili kujenga imani katika taasisi zenu na wadau wenu,”alisema.
Nae Naibu Katibu Mtendaji Idara ya Mipango Tume ya Taifa ya UNESCO, Aboud Idd Khamis, amesema maafisa wa habari ni moja ya rasilimali muhimu katika Taasisi hivyo kupitia mafunzo hayo yatawasaidia kuwaongezea uwezo na maarifa katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mkufunzi wa mafunzo hayo Imane Duwe alisema Maafisa wa habari pamoja na mambo mengine pia ana wajibu wa kushirikiana na watu, kujiamini pamoja na kujenga uthubutu.
Amesema maafisa pia wanapaswa kujua majukumu yao na kuwa wavumilivu sambamba na kuchakata data na kutoa taarifa za taasisi zao.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, ambapo mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo Ulinzi na Usalama kwa Waandishi na Maafisa Habari.