Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa (wa tatu kushoto) akipata maelezo ya Mradi wa Samia Haousing Scheme kutoka kwa mhandisi wa mradi huo Grace Musita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo tarehe 11 Septemba 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa akifafanua jambo kwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah (Kushoto) alipokwenda kukagua Mradi wa Samia Haousing Scheme uliopo Kawe jijini Dar es Salaam tarehe 11 Septemba 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa akitoka kukagua Mradi wa Samia Haousing Scheme uliopo Kawe tarehe 11 Septemba 2023. Kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa akiwa katika picha ya pamoja na wakandarasi wa mradi wa Samia Haousing Scheme uliopo Kawe jijini Dar es Salaam tarehe 11 Septemba 2023. Wa tano kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa akiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdalah kukagua mradi wa Morocco Square uliopo Morocco jijini Dar es Salaam tarehe 11 Septemba 2023.
Muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa Samia Housing Scheme uliopo Kawe jijini Dar es Salaam
(PICHA NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
…………………………
Na Sophia Kingimali
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amelitaka shirika la nyumba la Taifa(NHC) kuhakikisha mradi wa Samia Scheme unajengwa nchi nzima hasa katika miji mikubwa lakini pia kukamilisha miradi waliyoianzisha kwa wakati.
Hayo ameyasema Leo September 11 jijini Dar es salaam mara baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya shirika hilo ikiwemo mradi wa 711,Samia Scheme uliopo Kawe na Morroco Square.
Amesema idadi ya watu imeongezeka kulinganisha na awali hivyo NHC inapaswa kuwa na mpango wa kuwa na nyumba maeneo yote ili kupunguza changamoto kwa wananchi.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa la watu ukilinganisha na idadi ya nyumba zilizopo Sasa mnapaswa kuhakikisha mnajenga nyumba Kwa kulingana na idadi ya watu iliyopo”amesema Silaa
Amesema NHC wanapaswa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili waweze kuweka mitaji yao kwenye ujenzi na si kutegemea mikopo ya benki.
Amesema serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kisera ili kuhakikisha kunakuwa na ubia na watu au taasisi katika ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kuhusu mradi wa Samia Scheme(ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kuwauzia wananchi) uliogharimu bilioni 48 kwa nyumba 500 amesema mradi huo unapaswa kujengwa nchi nzima ili kuleta taswira nzuri ya nchi.
“Mradi huu unapaswa kujengwa nchi nzima hasa mkianza na miji mikubwa kama Dodoma idadi ya watu ni kubwa lakini nyumba za makazi ni chache”amesema Silaa
Mradi 711 amesema mradi huo unapaswa kuendelezwa ifikapo oktoba kwani ulisimama kwa muda ambapo mradi huo uligharimu kiasi Cha shilingi Bilioni 107.
Amesema mradi huo umesimama huku kukiwa na madeni hali inayopelekea kuongezeka kwa riba na gharama za uendeshaji.
“Mradi ulianzishwa muda mrefu wakati bei ya Saruji ya sasa ni tofauti na wakati bajeti ya mradi inaandaliwa”amesema Silaa
Akizungumzia mradi wa Morroco Square amesema mradi huo umegharim kiasi cha Bilioni 137 amesema mradi huo ni mkubwa na wa kwanza kwa NHC ambapo zàidi ya kaya 109 zitaishi hapo lakini pia maeneo ya biashara na huduma mbalimbali zitapatikana katika eneo moja.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutazalisha ajira lakini pia kuweka taswira nzuri ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa NHC Hamad Abdallah amesema kukamilika kwa mradi wa Morroco Square kutasaidia kuongezeka kwa mapato kwani kiasi cha Milion 850 kinatarajiwa kukusanywa kwa mwezi.
Amesema mradi huo umekua kivutio lakini chanzo kikubwa cha mapato ambapo mpaka Sasa umekamilika kwa asilimia 98.
“Huu ni mradi wa mfano hapa kulikua na nyumba tatu TU baada ya kufanya maboresho sasa hivi tunanyumba 100 za makazi,maduka makubwa lakini pia hoteli na majengo ya ofisi kwa hakika huu ni mradi wa mfano”amesema Abdallah
Akizungumzia miradi mingine amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati uliopangwa.
Ziara ya waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa shirika la nyumba la Taifa NHC imekuja ikiwa ni siku chache tu baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.