Na Sophia Kingimali
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa lengo ni kuvikuza vyama hivyo na si kutoa lugha za matusi kwa viongozi wengine au kukashifu chama chochote cha siasa.
Hayo ameyasema Leo Septembea 11 kwenye mkutano maalumu wa Baraza la vyama vya siasa na wadau wa demokrasia wenye lengo la kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi na Hali ya siasa nchini.
Amesema serikali kuruhusu mikutano hiyo ni hatua iliyichukuliwa kufuatia mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na Baraza.
Amesema licha ya kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa uhuru huo umeonekana kutumika kinyume na sheria za nchi pamoja na ubinadamu
“Kwa yeyote atakaebainika kuvunja Sheria hizo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria hii itasaidia kufuata sheria na kulinda utu wa mtu”amesema Dkt. Samia
Aidha Dkt. Samia amesema kuwa kuruhusu mikutano ya hadhara lengo lilikuwa ni vyama vitumie fursa hiyo kukua na kujijenga ikiwemo kurudisha wanachama walipotea kipindi mikutano hiyo iliposimama.
“Kuna baadhi ya vyama vya siasa vimetumia mikutano hiyo kutukana majukwaani,kuchambua dini za watu wengine na kukashfu mambo mbalimbali ya maendeleo hili sio lengo hasa la mikutano ya hadhara.”amesema Dkt. Samia
Akizungumzia Uhuru wa utoaji wa maoni juu ya demokrasia nchini Dkt. Samia amesema uhuru huu una mipaka yake si tu kisheria bali hata kibinadamu.
Akizungumzia katiba mpya Dkt. Samia amesema katiba ni ya watanzania wote hivyo lazima elimu itolewe kwa kila mwananchi.
Amesema mchakato huo unahitaji muda “maoni yaliyotolewa na wote wakikubaliana kufanya marekebisho ndiyo lengo litakuwa limetimia lakini niwakumbusha kuwa kazi hiyo ni mchakato inahitaji muda kuitengeneza lakini mtambue kuwa katiba ni mali ya watanzania wote si mali ya vyama vya siasa lazima elimu itolewe wananchi waijue sio kuwaburuza”amesema Dkt Samia
Sambamba na hayo Rais Dkt Samia amewataka viongozi wa dini kuanza kufundisha maadili kwa waumini wao hasa watoto ili kujenga misingi imara na kizazi chenye maadili.
Nae waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati akimkaribisha Rais Dkt. Samia amesema kila mtanzania anawajibu wa Kutunza amani na umoja uliopo ili kuendeleza mshikamano.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya wlWaziri mlMkuu Sera, Uratibu na Bunge Jenister Mhagama amesema mkutano huu wa siku tatu utafanya tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na vikosi kazi vyote viwili Bara na visiwani pamoja hali ya siasa hapa nchini na kuangalia uchaguzi ujao.
Nae mwenyekiti wa kituo cha Demokrasia nchi(TCD) Prof Ibrahim Lipumba ameomba kufanywa mabadiliko katika baadhi ya vifungu vya katiba kuelekea uchaguzi mkuu.