Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Bw. Adam Fimbo (wa pili kulia) akitoa ufafanuzi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto) wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kikazi leo Septembea 11, 2023 katika Ofisi za TMDA Jijini Dar es Salaam.
Kamati wa Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakiwa katika ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Jijini Dar es Salaam.
Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakisalimiana na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) baada ya kuwasili katika Ofisi za TMDA kwa ajili ya ziara ya kikazi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Bw. Adam Fimbo (wa pili kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI jinsi wanavyotoa huduma kwa njia ya mtandao.
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel (kulia) akipewa maelekezo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Bw. Adam Fimbo kuhusu vifaa vya Maabara ya Kimataifa ya TMDA vinavyofanya kazi.
Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakipewa elimu kuhusu Vifaa vya Maabara ya Kimataifa ya TMDA inavyofanya kazi.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetakiwa kuandaa mpango wa maboresha ya Maabara pamoja na kuhakikisha wafanyakazi wanatekeleza majukumu bila kuwa na kikwanzo jambo ambalo litasaidia kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta Maendeleo kwa Taifa.
Hata hiyo imekuja baada ya Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI leo Septemba 11, 2023 kufanya ziara katika Maabara ya TMDA iliyopo Jijini Dar es Salaam na kuridhishwa na utendaji kwa asilimia kubwa.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati wa Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo, amesema kuwa TMDA wamefanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija, hivyo wakati umefika wa kuandaa bajeti kwa ajili ya kuboresha maabara ili waendelee kufanya vizuri zaidi katika utendaji wao.
Mhe. Nyongo amesema kuwa kamati ina matumaini makubwa na TMDA kwa kuwalinda watanzania ili kuhakikisha wanakuwa usalama wa afya zao.
“Wananchi wanawategemea TMDA katika usalama wa afya zao, tuendelee kuwalinda katika kuhakikisha dawa na vifaa Tiba vinavyoingia sokoni zinakuwa na ubora” amesema Mhe. Nyongo.
Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha dawa zote zinazoingia sokoni zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
“Usalama wa dawa ni kitu nyeti, tunaomba chakula idhibitiwe na TMDA kwa sababu tuna imani nayo, kuna maabara yenye uwezo wa kimataifa na kufikia level four, duniani zipo maabara chache, serikali ifanya mabadiliko turudishe TMDA” amesema Mhe. Nyongo.
Hata hivyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa kuendelea kufanya maboresho katika sekta ya afya na kuwa imara.
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa katika wizara yake TMDA wamekuwa wakifanya vizuri katika kusimamia na kutekeleza majukumu yao kwa uweledi.
“Natoa pongezi kwa wafanyakazi WA TMDA kwa kufanya kazi vizuri, wakati mwengine tukiibiwa madawa hospital na kukosa ushaidi, lakini nikija kwa wataalamu wa TMDA wananisaidia na kunipa ushaida” amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wabunge pamoja na wadau mbalimbali katika kuimarisha TMDA ili kwenda pamoja na utaratibu wa Shirika la Afya Duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Bw. Adam Fimbo, amesema kuwa wanaendelea na kusimamia na kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuziondoa dawa feki katika soko.
Bw. Fimbo amesema pia wanaendelea kufanya maboresho katika nyanja mbalimbali ili kuongeza ufanisi wenye kuleta tija kwa Taifa.
“Ni jukumu letu kufatilia dawa baada ya kuisajili katika kipindi chote ambapo inatumika ili kuhakikisha yale matoleo yanayotengenezwa baada ya dawa kusajiliwa yanaendelea kukizi viwango vilivyowekwa” amesema Bw. Fimbo.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema kwa kushiriki na Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Halmashauri pamoja na timu za uendeshaji wa huduma za afya wanafatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha dawa feki hazipatikani katika soko.
“Tunaendelea kuzifatilia ili kuhakikisha dawa zilizopo zina ubora na zinakizi vigezo vyote vya ubora, pia tunahamasisha wananchi kutoa taarifa za dawa zozote ambazo zina madhara kwao” amesema Prof. Nagu.