………………………
Na Sixmund Begashe
Sekta binafsi zinazojishughulisha na Uhifadhi na Utalii nchini zimeshauriwa kutumia askari waliohitimu kutoka kwenye vyuo vya Uhifadhi chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa wamepata Mafunzo ya Taaluma hiyo
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abass, Jijini Mwanza kwenye mahafali ya 58 ya wahitimu wa mafunzo ya Uaskari wa Usimamizi wanyamapori na Himasheria, na Uongozaji na Usalama wa Watalii ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori -Pasiansi.
Dkt. Abbasi, ameongeza kuwa mafanikio ya filamu ya “Tanzania; The Royal Tour” ambayo Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki ili kuitangaza Tanzania yameendelea kuleta mafuriko ya mafanikio katika sekta hiyo, hivyo ni vyema wageni wanaoingia wakaendelea kuwa salama kupitia askari waliopikwa kwenye vyuo vya Wizara hiyo.
“Tayari kwa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania za Julai, 2022 hadi Julai, 2023 idadi ya watalii kutoka nje imefikia milioni 1.66 na mapato yamapaa hadi Dola za Marekani Bilioni 2.995 rekodi zote hizi hazijawahi kufikiwa wakati wowote katika historia ya nchi hii,” alisema Dkt. Abbasi.
Awali akitoa taarifa ya Chuo hicho Mkuu wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasisnsi, Bw. Jeremiah Timoth Msigwa amebainiisha kuwa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2022/2023 waliofaulu ni 349 kati ya 360 sawa na 96.9% ni sawa na ongezeko la ufaulu wa 2.06%. ikilinganishwa na mwaka wa masomo uliopita (2021/2022) ambapo wanafunzi waliofaulu ni 379 kati ya 399, sawa na 94.9%.
Ameongeza kuwa katika kuongeza wigo wa ajira kwa wahitimu wa Taasisi hii, na namna ya kukuza mapato, Taasisi hiyo mwaka 2020, ilianzisha mchakato wa kuwa na Kampuni ya Ulinzi, inayojulikana kwa jina la “Pasiansi Wildlife Security Company Ltd” (PASCO), Kipaumbele katika kutoa ajira kwa wahitimu wa chuo hicho.