JAMII Wilayani Kibaha , Mkoani Pwani imetakiwa kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye shughuli za maendeleo ili kuwe na haki sawa.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Ofisa Maendeleo ya Jamii kitengo cha jinsia wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Maria Nkangali wakati wa mafunzo kwa watu maarufu kwenye jamii kwenye kata ya Mkuza kupitia mradi wa uongozi wa wanawake na haki za kiuchumi (WLER).
Nkangali alieleza, lengo ni kufikia usawa wa kijinsia kwa asilimia 50 ambapo hadi sasa wamefikia asilimia 20.
“Lengo la mradi huu ni kuwa na usawa wa kijinsia kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uongozi, uchumi, umiliki wa ardhi na kupata huduma za kijamii,”alieleza Nkangali.
Nae Wakili wa Serikali kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha, Elizabeth Lukumay alifafanua baadhi ya ndoa zinakuwa ni batili kutokana na kutofuata taratibu za kisheria hivyo inapotokea zinavunjika mwanamke na watoto wanakosa haki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wazee kata ya Mkuza Anangisye Mwakapande alisema , changamoto za ndoa na ardhi ni kubwa kutokana na kutokuwa usawa wa kijinsia.
Mradi huo ni wa miaka mitano ulianza mwaka 2021 hadi mwaka 2026 ambapo mradi unatekelezwa kwenye kata tatu za Visiga, Mkuza na Pangani.