Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi wilayani Songea mkoani Ruvuma walipofanya utalii wa ndani katika bustani ya asili Ruhila mjini Songea.
……
Na Albano Midelo, Songea.
WANAFUNZI 800 wa shule mbalimbali wilayani Songea mkoani Ruvuma wametembelea bustani ya wanyamapori ya Ruhila iliyopo mjini Songea mkoani Ruvuma kwa lengo la kufanya utalii wa ndani.
Afisa Utalii wa Bustani ya asili Ruhila ambayo ipo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) David Tesha amesema wanafunzi hao walifika kutalii katika bustani hiyo katika kipindi cha kunzia Julai hadi Agosti mwaka huu.
“Maafisa uhifadhi wa Bustani ya Ruhila wamekuwa wanapita katika shule za msingi na sekondari mkoani Ruvuma kwa lengo la kutoa elimu ya utalii na uhifadhi,hali hiyo imechangia idadi kubwa ya wanafunzi kila mwezi kutembelea bustani yetu ya Ruhila’’.alisisitiza Tesha.
Amesema wanafunzi hao wakiwa katika bustani hiyo wameweza kutalii na kujifunza mambo mbalimbali ya uhifadhi na utalii Pamoja na kufurahia michezo ya kuendesha baskeli na michezo ya kubembea.
Hata hivyo amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2023 zaidi ya watalii 3,420 kutoka ndani na nje ya nchi wameweza kutembelea katika bustani ya Ruhila.
Amewataja watalii kutoka nje ya nchi ambao wametembelea katika bustani hiyo kuwa wanatoka katika nchi za Japan, Sweden,Norway,Nchi za Kiarabu,Nchi za Sikandinavia na Kenya na ametoa rai kwa watanzania kujenga utamaduni wa kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio vya utalii kama bustani ya wanyamapori Ruhila ambayo ipo mjini Songea.
Amewataja Wanyama ambao wanapatikana katika bustani hiyo kuwa ni simba,pundamilia, pofu, kakakuona, kuro, swalapala, sungura, nyumbu,jamii ya nyani ambapo amesema bustani hiyo ina madhari ya kuvutia yakiwemo maeneo mazuri ya kupigia picha na kuweka kambi kwa ajili ya utafitiBustani ya asili ya Ruhila ambayo ipo chini ya TAWA ilianzishwa mwaka 1973 na imekuwa inapokea watalii wa aina mbalimbali kutoka ndani ya nje ya nchi.