Na Sophia Kingimali
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amewakubusha viongozi wa Afrika kuendelea kuwekeza katika kilimo biashara ili kunusuru bara la Afrika kukumbwa na uhaba wa chakula kwani asilimia 65 ya ardhi Afrika inafaa kwa kilimo.
Kauli hiyo ametoa leo Septemba 7 jijini Dar es Salaam Dkt. Samia wakati akihutubia Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) mbele ya marais kutoka nchi mbalimbali kujadili juu ya nini kifanyike kuboresha mifumo ya chakula Afrika.
Amesema Jukwaa hilo la AGRF litatoa na suluhu ya changamoto ya chakula na viongozi wa Afrika wapo tayari kuhakikisha Afrika inajitosheleza Kwa chakula
“Asilimia 60 ni vijana ambao ni nguvu kazi na sisi viongozi wa Afrika tupo tayari kuondoa aibu ya Afrika kuwa walalamikaji tupo tayari kulisha Afrika na duniani kwa ujumla, ” amesema Dk. Samia.
Amesema licha ya rasilimali zilizopo Afrika wamebaki kuwa walalamikaji badala ya kutafuta suluhisho kuelekea njia ya mapinduzi ya uchumi wa kijani.
” Tupo na AGRF washiriki wa maendeleo sekta binafsi wasomi na wataalamu kubadilishana uzoefu namna ya kuboresha mnyororo wa thamani ya bidhaa za kilimo na kujadili mipango ya kuimarisha usalama wa Chakula Afrika, ” amesema.
Amesema kuelekea mageuzi wanayotaka katika sekta ya kilimo ni muhimu viongozi kwa pamoja tukaweka mipango na mikakati kufikia Afrika tunayoitaka.
Aidha amesema ili kufikia malengo viongozi wa Afrika hawana budi kufanya tathimini ya vipaumbele vyao wavioanishe na mahitaji ya sasa katika muktadha wa dunia ambapo imeeleswa kuwa zaidi ya watu milioni 283 wanalala njaa barani Afrika.
Nae Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto amesema ardhi ya kilimo ipo Afrika mkutano huo wa AGRF ni somo kubwa hivyo Teknolojia na muda unahitajika ili kuweza kupata chakula Cha kutosha kwenye bara la Afrika hata kupeleka Duniani.
” Tunaweza kuchochea biashara ya kilimo kuacha kuwa watu wa kulalamika wakati ardhi tunayo ni suala la kuongeza uzalishaji na kufikiria tunafanyeje wakulima wazalishe zaidi,” amesema Rais Ruto.
Amesema katika somo la mkutano huo wa AGRF ni jinsi gani watafanya mabadiliko ili kubadilisha wakulima waweze kuzalisha Kwa wingi ili gharama za chakula zipungue.