Mbunge wa Jimbo la Singida, Magharibi, Elibariki Kingu,
………………………………………………..
Na Dotto Mwaibale, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, amemshukuru Rais
Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara ya kutoka Sepuka wilayani Ikungi hadi Kizaga wilayani Iramba ambayo ujenzi wake unatarajia kuzinduliwa kesho kutwa Septemba 9, 2023.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana alisema hana la
kusema zaidi ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mungu ampe afya na maisha marefu ili aweze kuendelea kuliongoza taifa letu la Tanzania.
” Naishiwa maneno ya kumueleza Rais Samia mama mwenye huruma na upendo kwa watanzania ambaye anakwenda kuyabadilisha maisha ya wana Singida Magharibi,
Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla kutokana na kazi yake hii kubwa iliyotukuka,” alisema Kingu.
Kingu alisema uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kufanyika
Septemba 9, 2023 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ambapo pia atakuwepo Waziri wa Fedha, Dk.Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi..
Pia hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.
Kingu alisema kilio chake na hoja yake kubwa tangu ameingia bungeni ilikuwa ni ujenzi wa barabara hiyo na kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kukisikia.
” Toka mwaka 2015 nimekua nikipigania barabara hii na sasa yametimia, lakini ile ya Iyumbu hadi Tabora kupitia
Singida nimeanza mwaka huu na tayari tumepewa pesa za kufanya upembuzi yakinifu,” alisema Kingu huku akionesha tabasamu la furaha.
Aidha, Kingu alisema ujenzi wa barabara ya Singida Sepuka hadi Kizaga itafufua ukuaji wa uchumi katika Jimbo la Singida Magharibi na Mkoa wa Singida kwa ujumla.
Kingu alitoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo waendelee kuunga mkono jitihada za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuupokea mradi huo kwa heshima
kubwa na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi watakao kuwa wanajenga..