Katibu Bakwata wilaya ya Arusha jiji ,Banka Seif Banka Banka akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mikopo hiyo.
Qadhi wa wilaya ya Arusha jiji ,Shehe Abdulrahman Salum akizungumza jiji Arusha.
…..
Julieth Lazier, Arusha.
BAKWATA wilaya ya Arusha jiji imekabithi mkopo wa shs 4 milioni kwa wanawake wajane na wanaoishi kwenye mazingira magumu wapatao 20 ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili.
Akizungumza wakati kukabithi fedha hizo kwa wanawake hao,Katibu wa Bakwata wilaya ya Arusha jiji,Banka Seif Banka amesema kuwa wamefikia hatua ya kufanya hivyo kwa lengo la kuwasaidia wanawake wajane na wenye hali duni ili waweze kuboresha mitaji ya biashara na kuongeza kipato chao.
“Fedha hizo tulizowapa leo hii watarejesha kwa muda wa miezi mitano hadi sita ili kuwawezesha wengine wenye mahitaji hayo kuweza kukopa na mkopo huu hauna riba yoyote ,hivyo nawaomba mkatumie kwa malengo yaliyokusudiwa mrudishe kwa wakati ili na wengine waweze kufikia.”amesema Banka .
Aidha amesema kuwa, kwa kuanzia wameanza na wanawake 20 ambapo wataendelea kutoa kwa wanawake wengine wenye hali duni na wajane ili waweze kuendeleza biashara zao na kuondokana na changamoto mbalimbali.
Aidha Banka amezitaka taasisi zingine kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wanawake wenye mahitaji maalumu kwani wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali za maisha .
“Hawa wanawake tuliowasaidia wamekuwa wakifika ofisini kwetu mara kwa mara kwa lengo la kuomba kuwezeshwa ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha shughuli ndogondogo ambazo zitawaingizia kipato na kuondokana kuwa tegemezi ndo maana tukaamua kuwakopesha kila mmoja shs laki mbili fedha isiyokuwa na riba.”amesema .
Kwa upande wake mgeni rasmi katika halfa hiyo Naibu Qadhi Mkuu Tanzania ,Sheikh Ally Ngeruko amewataka wanawake hao kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika urejeshaji wa mikopo hiyo ili na wengine waweze kunufaika na kujikwamua kiuchumi kwani kadri watakavyorejesha kwa wakati ndivyo na wengine watakavyoweza kupata mikopo hiyo.
Naye Qadhi wa wilaya ya Arusha jiji,Sheikh Abdulrahman Salum amewataka wanawake hao kuitumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kwenda kuitumia kwa mambo yasiyofaa kwani kwa kufanya hivyo itawawia vigumu katika kufikia malengo yao waliyojiwekea.
“Kitendo kilichofanywa na Bakwata ni mfano wa kuigwa kwani ni njia mojawapo ya kuiunga mkono serikali katika maswala mbalimbali ya maendeleo na kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi ,hivyo nawaomba wanawake hawa wakawe waaminifu na kuheshimu makubaliano yaliyowekwa. “amesema.
Nao baadhi ya wanawake hao waliopatiwa mikopo hiyo Amina Juma na Hamida Hamis wameshukuru Baraza hilo kwa namna ambavyo litawasaidia kwani fedha hizo zitawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili huku wakiahidi kurejesha kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo.