Na. WAF, Dodoma
Tanzania ina jumla ya Madaktari Bingwa Wazalendo 2,469 ambao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika wa fani mbalimbali za Udaktari Bingwa.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Molel wakati akijibu swali namba 103 la Mhe. Angelina Adamu Malembeka (VITI MAALUM) aliyeuliza Tanzania ina Madaktari Bingwa Wazalendo wa magonjwa ya Binadamu wangapi na katika magonjwa gani, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu bungeni leo Jijini Dodoma
Mhe. Godwin Mollel amesema kuwa kati yao Madaktari Bingwa 2,098 wapo katika Sekta ya Umma na Madaktari Bingwa 371 wapo Sekta Binafsi.
Amesema madaktari hao wamegawanyika katika maeneo 28 ya Ubingwa kwa lengo la kutoa Huduma kwa wananchi.
Dkt. Mollel akijibu swali namba 104 kutoka kwa Mhe. Jacquiline Ngonyani Msongozi aliyeuliza lin Serikali itatoa fidia kwa Madaktari na Manesi wanaopoteza maisha wakihudumia Wagonjwa wa Magonjwa ya Mlipuko ambapo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kujali mchango mkubwa wa Watumishi wanaohudumia wagonjwa wa magonjwa ya milipuko wakiwemo madaktari na wauguzi.
“Napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba Serikali hutoa fidia kwa watumishi waliofariki kwa sababu za kuwahudumia wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko kwa Sheria ya Fidia kwa wafanyakazi Sura ya 263 marejeo ya Mwaka 2015 kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Tanzania”. Ameeleza Dkt. Mollel .
Ameeleza kuwa fidia zinazotolewa kwa mtumishi wa afya wakati anapopata changamoto ni pamoja na gharama za mazishi na pensheni kwa wategemezi wake.
Hata hivyo amewapongeza watumishi wa afya kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma za afya kwa wananchi ili kuhakikisha taifa linakuwa salama