Na Sophia Kingimali
Katika kukuza na kuboresha sekta ya kilimo Benki ya Dunia imetoa mkopo wa Dola milioni 300 za Marekani,ambazo ni sawa na zaidi ya sh bilion 700,kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa wakulima wadogo hapa nchini.
Hayo ameyasema Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati wa uzinduzi wa programu ya Mpango wa kustahimili Mifumo ya chakula nchini,uliofanyika jana jijini Dar es salaam,katika mkutano wa pembeni ya mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF).unaendelea .
“Fedha hizi ni mkopo wa muda mrefu kwa serikali zitatumika ndani ya miaka mitano kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kilimo,ikiwemo uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya wakulima wadogo lakini Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii tutajitahid mradi tuufanye Kwa miaka mitatu tu”amesema Bashe
Amesema fedha zinakwenda kufanya kazi katika hekta 37,000 ambazo zimetengwa kwa ajili ya Kilimo cha umwagiliaji ambacho vijana wengi wamehamasishwa kuingia kwenye Kilimo hicho.
Bashe amesema kabla ya utoaji wa fedha hizo,walikaa kikao kujadili kuhusu matumizi ya fedha hizo ambazo zimetolewa na Benki ya dunia kwa mara ya kwenye sekta ya Kilimo.
“Tunaishkuru sana serikali kwa kuridhia mkopo huu kwenye sekta ya kilimo,naamini zinakwenda kuleta matokeo chanya kwenye Kilimo cha umwagiliaji ikiwemo kulinufaisha taifa,”alisema Bashe.
Aidha Waziri Bashe amewataka watanzania kujikita kwenye Kilimo kama wanavyofanya katika suala la mazingira ili kuhakikisha kilimo kinakubalika kwa jamii.
Kwa upande Waziri wa Kilimo umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamanta Shaame Khamis ameishkuru serikali kutokana na kuanzisha programu hiyo ambayo inakwenda kuwainua wakulima nchini
Amesema kwa upande wa Zanzibar watakwenda kuboresha miundombinu mbalimbali ya kilimo ili kuhakikisha kilimo kinapiga hatua na kuwainua wakulima kiuchumi wao na familia zao.
Aidha amempongeza Bashe kutokana na kubuni mradi huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huku akisisitiza taifa linakwenda kuinuka kupitia Kilimo.
Amesema mradi huo ni sehemu muhimu sana kwao kwa sababu wanakwenda kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika hekta ambazo zimetengwa kwa ajili ya Kilimo hicho.
Awali akiwakaribisha wazungumzaji Katibu Mkuu wawizara ya Kilimo Gerald Mweri amesema anaishkuru AGRF kwa kushirikiana na serikali kuandaa mkutano huo ambao unakwenda kuleta manufaa makubwa kwa taifa na wakulima kwa ujumla.
Mweri amesema wakulima na wafanyabiashara wanapaswa kutumia fursa hiyo ambayo imetolewa na serikali kwa ajili ya kupiga hatua katika shughuli za kilimo wanazofanya.