*Zaidi ya Shilingi bilioni 52 zimetolewa na Migodi tangu kutungwa kwa Kanuni za CSR, 2018 – 2022
*GST kujengewa uwezo kufanya tafiti za kina
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameahidi kuipa ushirikiano Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika kutekeleza majukumu yake ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye maendeleo ya nchi.
Ameyasema hayo leo Septemba 5, 2023 alipokutana na Kamati hiyo jijini Dodoma ili kuzungumzia mwenendo wa biashara na shughuli za Sekta ya Madini sambamba na kufahamiana na Kamati baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Madini.
“Ninawaahidi kuwapa ushirikiano katika kipindi chote ninyi kama Kamati ya Bunge ili kwa pamoja tushirikiane katika mageuzi haya kwenye Sekta hii muhimu hapa nchini,” amesema Mhe. Mavunde.
Pia, Mhe. Mavunde ameieleza Kamati hiyo kuwa Wizara imeandaa mpango wa kuiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia Tanzania (GST) kwa kuipatia vifaa na teknolojia ya kisasa zaidi ili ifanye utafiti wa kutosha kuendana na mahitaji ya sasa ya Dunia na kuibua maeneo mengi zaidi yaliyo na madini hapa nchini ili kuongeza wigo wa Sekta hiyo sambamba na mchango wake katika Pato la Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ussi Pondeza amesisitiza kuwa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini itatoa ushirikiano kwa Waziri Mavunde na timu yake ili Sekta ya Madini iwanufaishe Watanzania kupitia uchumi wa madini.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesisitiza kuwa, maelezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo hususan ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini na Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) yatafanyiwa kazi na Wizara ili Sekta ya Madini isonge mbele.
Naye, Kaimu Afisa Biashara Tume ya Madini, Alfa Edward akiwasilisha mada kuhusu Usimamizi biashara ya Madini nchini amesema biashara ya Madini imezidi kuimarika baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanyika Mwaka 2017 na kupelekea uanzishwaji wa masoko ya madini kutoka 25 mwaka 2018/2019 hadi 42 kwa mwaka 2022/2023 na vituo vya ununuzi viwili (2) mwaka 2018/2019 hadi 94 kwa mwaka 2022/2023.
“Mabadiliko ya Sheria yamesababisha ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na kupungua kwa utoroshaji na biashara haramu ya madini,” amesema Edward.
Aidha, ameeleza Kamati hiyo historia fupi ya biashara ya madini nchini, aina za madini yanayopatikana nchini, jukumu la Tume ya Madini katika Biashara ya Madini, Mfumo wa Usimamizi biashara ya madini na mafanikio ya biashara ya madini.
Kwa upande wake, Afisa Biashara Tume ya Madini, Issa Lunda akifafanua kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) ameeleza kiasi au asilimia ya malighafi zinazozalishwa, wafanyakazi, fedha, bidhaa na huduma zinazotolewa na kutumika katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
“Lengo la makusanyo kwa mwaka 2022/2023 ni Shilingi Bilioni 822.02 sawa na wastani wa Bilioni 68.50 kwa mwezi, Mh. Mwenyekiti katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2023, jumla ya kiasi cha Shilingi Bilioni 678.04 kimekusanywa, makusanyo hayo ni sawa na asilimia 82.49 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2022/2023.” ameongeza Lunda.
Vile vile, amesema zaidi ya shilingi bilioni 52 zimetumika na kutengwa na migodi mbalimbali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii tangu kuanzishwa Sheria ya CSR Mwaka 2018 – 2022.
Kikao hicho kifupi kimehudhuriwa na Wajumbe wa Kamati hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali, Wakuu wa taasisi na Viongozi wa Wizara na Taasisi zilizopo chini ya Wizara.