Wanawake wa Kabila la Kimasai walioshiriki Mkutano Mkuu Maalumu wa kuanzisha Jukwaa la Wanawake wa Vijijini Tawi la Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa Mkutano huo uliofanyika Mkoani Mbeya ukiwashirikisha wajumbe kutoka mikoa iliyopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini waliowawakilisha wenzao kitaifa.(Picha na Joachim Nyambo)
Na Joachim Nyambo, Mbeya.
WANAWAKE wa Kabila la wafugaji la Kimasai wamesema ujio wa Jukwaa la wanawake wa Vijijini ni fursa nyingine inayopaswa kutumika kuwakomboa wanawake walio katika makabila ya wafugaji kutuokana na changamoto nyingi za ukatili wa kijinsia zinazowakabili.
Miongoni mwa changamoto walizozitaja ni pamoja na wanawake kunyimwa fursa ya kumiliki rasilimali ikiwemo ardhi pamoja na mifugo licha ya kuwa wazalishaji wakubwa katika familia zao.
Wanawake wa kabila hilo waliyasema hayo katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi baada ya kuanzishwa kwa Jukwaa la Wanawake wa Vijijini Tawi la Tanzania.
Mmoja wa wanawake hao, Eloy Satulo kutoka Kijiji cha Matebete kilichopo katika Kata ya Itamboleo wilayani Mbarali mkoani Mbeya alisema changamoto kubwa bado juhudi za ziada zinahitajika ili kumweka huru mwanamke wa kimasai na jamii nyingine za wafugaji ili kumfanya anufaike na rasilimali zilizopo kwenye eneo lake kama ilivyo kwa mwanaume.
“Changamoto kubwa ni kuwa wanawake katika jamii za kifugaji hasa kwa sisi wamasai wengi hatumiliki rasilimali…na tunaposema rasilimali ni pamoja na ardhi. Na pia hata hiyo mifugo tunayofuga ni miliki ya wanaume..maana yake hata kwenye familia akiitwa huyu ng’ombe ni wa kwako inabakia ni jina tu ila masuala mengine wewe hayatokuhusu.” Alisema Eloy
“Kuna wanawake wengine wanaweza kuwa wanajihusisha na kilimo kama sehemu ya kuweza kujikimu lakini anayeweza kufanya maamuzi juu ya hicho kinachofanyika au mauzo ya mavuno ni mwanaume.” Aliongeza
Eloy ambaye kupitia Mkutano huo maalumu alibahatika kuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza watakaoongoza Jukwaa hilo kitaifa kwa mwaka mmoja akishika nafasi ya Katibu Mkuu Kitaifa alisema pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali nchini kwa kusaidiana na wadau mbalimbali katika kumkomboa mwanamke bado kuna vikwazo.
“Tunaposema ujio wa Jukwaa hili ni fursa kwa sababu tunaamini kadiri tunavyozidi kupata elimu wengine wanazidi kufunguliwa na unapofanya kitu kizuri hata kama Yule mwanaume alikuwa analeta vikwazo kuna namna anazidi kupunguza.”
Naye Truket Akasho, Mwanamke kutoka kabila la wamasai pia mkazi wa Kijiji cha Mwanavala Kata ya Imalilo Songwe wilayani Mbarali alisema Jukwaa litakuwa chachu na lenye msaada mkubwa kwa wanawake vijijini iwapo kazi zake zitajikita maeneo ya pembezoni kama ilivyo malengo yake.
Truket ambaye pia ni miongoni mwa wanawake wanufaika wa nafasi ya udiwani viti maalumu wilayani Mbarali mkoani Mbeya alisema atahakikisha jukwaa hilo linafika hadi katika vijiji vinavyomzunguka. Si mara ya kwanza kwake kwani amekuwa akifanya juhudi mbalimbali za kuwakomboa wanawake wa kabila hilo.
“Mimi nimefika hapa kama mwakilishi wao, nitapeleka huu ujumbe. Tuna majukwaa kijijini na nina vikundi vya wanawake wenzangu ambavyo nimekuwa nikifanya navyo kazi vijijini. Kupitia vikundi wanawake wananufaika kupitia ujasiriamali.”
“Sisi ni wafugaji tumeunda vikundi tunafuga mbuzi wa biashara, tunanunua kama ni dume wanakuwa wadogowadogo baada ya miezi sita wakikua tunawauza. Na kuna wakati tunanunua mbuzi jike wakubwa na madume tunazalisha.”
Lakini alisema jambo kubwa sasa wanalokwenda kulipa uzito ni suala la wanawake kumiliki ardhi na kuwasihi wanawake wa kabila hilo kutosita kujiunga na Jukwaa pale watakapofikiwa.
“Kuna migogoro mingi kule ya ardhi..tuna mgogoro wa hifadhi kuwa ardhi yetu inakwenda kuwa chini ya hifadhi. Hata kijiji ninachotoka mimi watu tayari wamefanyiwa tathimini hivyo wanapaswa kuondoka. Nitatoa elimu ili hata kama mtu anahama atakakokwenda ardhi akaimiliki kisheria na wanawake wakiwemo.” Aliahidi Truket.
Jukwaa la Wanawake Vijijini(Rural Women’s Assembly) kwa mataifa mengine yaliyopo Ukanda wa Kusini mwa Afika yaani nchi za SADC lilikuwepo. Yapo mataifa kama Afrika Kusini ambayo tayari jukwaa hili lina zaidi ya miaka 10 hadi sasa.
Ni Jukwaa linalolenga kuwezesha wanawake kujikita katika agenda kuu muhimu za Ardhi,Kilimo Ikolojia,Ukatili wa Kijinsia na Mabadiliko ya tabia ya nchi. Lengo ni kuwapa mwamko zaidi wa kuwa na ushiriki mkubwa kwenye maeneo hayo muhimu ndani ya jamii.