Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari wa kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu nchini Tanzania (OJADACT)Edwin Soko akizungumza na waandishi wa habari juu ya umuhmu wa warsha iliyowakutanisha waandishi wa habari na Azaki.
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Internews Agnes Kayuni akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya siku mbili kwa Waandishi wa habari na Asasi za kiraia.
Waandishi wa habari na Azaki wakiendelea na mafunzo.
……….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la kimataifa la Internews limefanya warsha iliyowakutanisha waandishi wa habari na Asasi za kiraia (AZAKI) kwaajili ya kuwajengea uwezo wa kufanya kazi zao kwa ufanisi pamoja na kuwa na mahusiano mazuri ya kazi hatua itakayosaidia kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.
Warsha hiyo imefanyika leo Jumatatu Septemba 4, 2024 Jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo itakayofanyika kwa siku mbili Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Internews Agnes Kayuni, amesema katika tathimni mbalimbali walizozifanya wamegundua kuna ukosefu wa uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi ndio maana wanatoa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo mkubwa utakao wasaidia katika utendaji wao wa kazi.
“Kwa upande wa AZAKI tunatoa mafunzo ya wao kuweza kutumia vyombo vya habari ili kazi zao ziwafikie walengwa hatua inayosaidia kuchochea maendeleo ya Taifa, kwa waandishi wa habari tunawapa mafunzo ili wafanye kazi zao kwa weledi ikiwemo kuzingatia misingi iliyopo sanjari na kuepuka na kuandika habari za upande mmoja”, amesema Kayuni.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kupata mtandao utakao wasaidia kushirikiana na kuangalia changamoto zilizopo ambazo wanaweza kuzipatia ufumbuzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari wa kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu nchini Tanzania (OJADACT) Edwin Soko, amelishukuru Shirika la Internews kwa kuleta mafunzo hayo yatakayo boresha mahusiano baina ya AZAKI na Vyombo vya habari.
Amesema kunaudhaifu kidogo wa mawasiliano kati ya Azaki na vyombo vya habari hivyo kupitia mafunzo hayo anaamini kutakuwepo na mabadiliko yenye tija yatakayojenga mahusiano ya kudumu.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Farijika Community Development And Rights Organization Aisha Mtumwa amesema mafunzo aliyoyapata yatamsaidia kufanya kazi zake kwakushirikiana na vyombo vya habari.