Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kufanya uchunguzi kuhusu mradi wa maji wa Sh. bilioni 1 uliokuwa ukitekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika vitongoji 7 vya Kata ya Vumari.
DC Kasilda ametoa maagizo hayo wakati alipokwenda kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa wilayani humo, ikiwemo miradi ya maji, ujenzi wa Madarasa ya shule ya msingi Mbono unaotekelezwa na Mradi wa Boost utakaogharimu jumla ya Sh. Millioni 181.
“Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amejitahidi kutoa fedha nyingi Sana kwa ajiri ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali ikiwemo hii ya Maji ambapo ametoa Sh. Bilioni 1 kwa ajili ya ukamilishwaji katika vitongoji hivyo 7,” Amesema Kasilda.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa imekuwa ni usimamizi mbovu wa Miradi ambapo Wananchi wanashindwa kunufaika na miradi hiyo kutokana na uzembe amesema Mkuu wa wilaya huyo.
“Takukuru naomba mfuatilie haraka iwezekanavyo na kuchunguza hili tujue ni kitu gani kinachofanya wananchi hawa wa vitongoji vitano kati ya saba wasinufaike na miradi ya maji na ni kwanini maji hayawafikii wananchi hao.
Pamoja na Hayo yote Mkuu wa wilaya Kaslida Mgeni ametoa shukrani za dhati kwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kuipatia Same fedha nyingi kwa ajiri ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhakikisha fedha zinazo tolewa na Serikali zinatumika vyema kwa kutekeleza miradi inayokusudiwa
Pia meneja wa maji wilaya ya Same Abdallah Gendaheka amesema kukosekana kwa maji katika vitongoji vitano ni kutokana na bahadhi ya wananchi kuharibu miundombinu ya maji na vifaa vya maji.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Vumali Wilayani humo Asha Abdallah na Herman Mgonja wamesema changamoto kubwa wanayopata ni maji hasa kwenye hiki kipindi cha kiangazi ambacho wanalazimika kunywa maji yasiyo safi na salama