Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia bibi mmoja aitwaye MALOGI LUOBELA [75] Mkazi wa Kijiji cha Ikoho Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa tuhuma za kumuua mjukuu wake aitwaye VISION ERICK mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitano kwa kumkata kwa jembe.
Ni kwamba Agosti 31, 2023 majira ya saa 4:30 asubuhi huko Kitongoji cha Mapinduzi, Kijiji cha Ikoho, Kata ya Maendeleo, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini, mtoto VISION ERICK, mwaka mmoja na miezi mitano alifariki dunia baada ya kukatwa kwa jembe kichwani na Bibi yake aitwaye MALOGI LUOBELO [75] Mkazi wa Ikoho.
Chanzo cha tukio hili ni mtuhumiwa alikuwa anachimba udongo ili kukandika katika nyumba na ndipo wakati anaendelea mtoto huyu alitambaa hadi eneo hilo bila mtuhumiwa kumuona kutokana na hali yake ya uono hafifu [upofu] na ndipo alimkata kwa jembe kichwani na kusababisha kifo chake.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamsaka dereva wa Gari yenye namba za usajili T.436 CGD aina ya Mitsubishi Canter mali ya kampuni ya Mainland Pharmacy Center aitwaye KHADHAR IDD ADAMU [28] Mkazi wa Mkoa wa Katavi – Mpanda, mwenye asili ya Kisomalia kwa tuhuma za kumgonga kwa Gari askari wa Kikosi cha usalama barabarani WP.2645 S/SGT ZAINA akiwa katika majukumu yake.
Ni kwamba, Agosti 30, 2023 majira ya saa 11:40 jioni huko eneo la Kabwe Jijini Mbeya katika Barabara kuu ya Mbeya – Njombe, Gari T.436 CGD Mitsubishi Canter ikiendesha na KHADHAR IDD ADAMU [28] alimgonga askari wa kikosi cha usalama barabarani WP.2645 S/SGT ZAINA alikuwa kazini akitekeleza majukumu yake ya kuvusha watembea kwa miguu Barabara na kumsababishia maumivu sehemu za kiunoni na mgongoni.
Chanzo cha ajali ni Dereva wa gari kuendesha Gari kwa uzembe na kushindwa kuchukua tahadhari kwenye maeneo ya makazi na mkusanyiko wa watu wengi. Mtuhumiwa anaendelea kutafutwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawatangazia wananchi wote kusalimisha silaha haramu kwa hiari katika vituo vya Polisi vilivyopo Jirani nao, ofisi za serikali kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa kuanzia Septemba 01, 2023 hadi Oktoba 31, 2023.
Zoezi la usalimishaji silaha haramu kwa hiari litafanyika kwa kipindi cha miezi miwili. Kwa mwananchi yeyote atakayesalimisha silaha haramu kwa kipindi hiki hatakamatwa wala kuchukuliwa hatua zozote za kisheria. Usalimishaji wa silaha utafanyika kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika maeneo yaliyotajwa hapo juu.
Imetolewa na:
BENJAMIN KUZAGA
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.