Na Sophia Kingimali,Dar es salaam
Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wametakiwa kupeleka elimu ya matokeo ya sensa kwa wananchi pamoja na kutumia matokeo hayo katika kupanga shughuli za maendeleo katika mikoa
Hayo ameyasema Leo jijini Dar es Salaam Agosti 31 wakati wa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa kwa wakuu hao wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kamisaa wa sensa Anna Makinda amesema viongozi hao wanapaswa kutumia matokeo ya sensa katika kupanga shughuli za kimaendeleo katika mikoa Yao pamoja na kutoa elimu ya sensa Kwa wananchi
Makinda amesema kuhesabu watu siyo mwisho, kazi kubwa iliyopo mbèle yao na viongozi hao ni kupeleka elimu ya matokeo hayo ya sensa kwa wananchi ili waweze kuyaelewa na kuyatumia katika mipango hiyo ya maendeleo kwenye maeneo yao.
“Sisi wenyewe hatuwezi kumaliza nchi nzima kutoa elimu hii ya matokeo ya sensa, tunawategemea viongozi hawa na kamati zao za sensa kuyachukua haya na kuyapeleka kwa wananchi, bahati nzuri katika takwimu zetu zipo za hesabu ” alisema Makinda
Aidha amesema bidii, ubunifu na kujituma kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala kumefanya zoezi hilo la sensa kuendeshwa kwa urahisi na kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa amesema wanawashukuru wakuu wa mikoa kwa kutekeleza na kutoa ushirikiano katika kukamilisha zoezi sensa ya watu na makazi lililofanyika Oktoba mwaka jana.
Hata hivyo Dk. Chuwa amesema matokeo ya sensa hiyo yameonesha kuwa umri wa mtanzania kuishi umeongezeka kutoka miaka 44 hadi 65 na kwamba hizo ni juhudi ambazo zinafanywa na wakuu hao wa mikoa katika kumsaidia Rais kwenye utendaji kazi wake.
Awali akizungumza kwa niaba Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema lengo la mafunzo ni kutumia matokeo hayo ya sensa ya mwaka 2022 katika kupanga, kupima na kutahimini utekelezaji wa maendeleo.
“Lakini pia yataongeza uelewa wa kutosha wa matumizi wa matokeo ya sensa, sisi kama viongozi wa mikoa matokeo haya yatatusaidia katika kufanya maamuzi ya kitakwimu yanayoakisi hali halisi ya mahitaji ya wananchi,” amesema Telack na kuongeza
“Kama tunavyofahamu suala la kupanga maendeleo ni shirikishi na linaanzia kwa wakuu wa mikoa kuanzia vijiji mpaka juu, hivyo kupitia mafunzo haya yatatuongezea ujuzi na uzoefu katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku,” amesema