Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi – TUCTA wamepongeza ushirikishwaji wa wadau unaofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika kujadili na kupata maoni mbalimbali yanayohusiana na huduma za Mfuko huo.
Haya yamesemwa na Rais wa TUCTA Bw. Tumaini Nyamhokya wakati wa mkutano wa NHIF na shirikisho hilo uliofanyika leo jijini Arusha wenye lengo la kushirikisha wadau hao katika kujadili masuala mbalimbali ambayo yanachangia katika uimarishaji wa huduma za Mfuko huo.
“NHIF imetushirikisha mafanikio na changamoto za huduma na mkutano huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliopo hapa wamekuwa wawazi na wametoa maoni, mrejesho wa huduma kwa niaba ya wafayakazi nchini na naamini kwamba ushirikishwaji huu una nafasi chanya katika maendeleo ya Mfuko huu” amesema Bw. Nyamhokya.
Mkutano huo ni mwendelezo wa utaratibu wa NHIF wa kukutana na wadau wake ikiwemo wanachama, watoa huduma za matibabu, wawakilishi wa wananchi na makundi mbalimbali. Katika mwendelezo huu, Mfuko huo umeshakutana na wadau wake wa mikoa ya Singida, Mwanza, Geita,Tabora, Rukwa, Mtwara na Njombe na Dar es Salaam kwa kipindi cha kuanzia Julai mwaka huu.
Awali akiongea wakati wa kuwasilisha mada ya Mfuko huo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga alisema Mfuko huo unafanya hivyo kwa kuwa wadau wake ndio nguzo katika maendeleo yake na wanachama wake wengi ni watumishi.
“Tunathamini ushirikishwaji kwa sababu wadau ndio wanafanya uwepo wa Mfuko huu, tunapata mrejesho wa huduma kutoka kwa wanachama, watoa huduma za matibabu ndio wanaotibu wanachama wetu hivyo nao tunakutana nao mara kwa mara, ndio maana tumeona umuhimu wa kukutana nanyi kama shirikisho mnaowakilisha watumishi wa umma na binafsi” amesema Bw. Konga.
Kwa upande wao wajumbe wa mkutano huo ambao ni wawakilishi wa vyama takribani 13 vya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi walipongeza juhudi zinazofanywa na Mfuko huo katika kuwahudumia watumishi nchini lakini pia kutoa nafasi ya kuwashirikisha kutoa maoni na kutoa mrejesho wa huduma.