NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
BENKI ya NMB imemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwamba itaendelea kuwa mdau kinara wa Serikali yake katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Watanzania.
Ahadi hiyo imetolewa jana Agosti 31 na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Ruth Zaipuna, wakati akitoa shukrani na salamu kwa Rais Samia, wakati akifunga Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2023), lililofanyika kwa wiki moja kwenye Viwanja vya Paje, Mkoa wa Kusini Unguja.
Kizimkazi Festival limekuwa likitumika kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), pamoja na wadau zikiwemo taasisi binafsi, ambako Rais Samia alizindua miradi miwili mikubwa (Agosti 29 na 30) iliyofanywa na NMB.
Bi. Zaipuna alimhakikishia Rais Samia kwamba, NMB itabaki mstari wa mbele katika kusapoti jitihada zake na zile za Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi za kuwaletea maendeleo Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla, huku akibainisha kuwa miradi miwili iliyozinduliwa kupitia tamasha hilo, itatoa mchango mkubwa wa maisha bora kielimu na kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
“Jana (Agosti 30), tumezindua Tawi la NMB Paje, ambalo umelizindua wewe mwenyewe, tunaamini tawi hili linaenda kuwa suluhu ya changamoto za huduma za kibenki walizokuwa wanakabiliana nazo wakazi wa Paje, ambao walilazimika kusafiri kilomita 60 kufuata huduma hizo katika tawi letu la Mwanakwerekwe.
“Tunaamini ujio wa Tawi la NMB Paje, utachagiza ongezeko la Watanzania wanaotumia huduma za kibenki, ambao kwa takwimu zilizopo sasa wapo asilimia 22 tu. NMB tunalitambua hilo, ndio maana kupitia tawi hili, tutatoa elimu ya fedha kwa wananchi, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi na wajasiriamali.
“Kama tunavyofanya popote tunapofungua tawi jipya, kutoa sehemu ya faida yetu kupitia Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), hapa Kusini Unguja wewe mwenyewe umeweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Skuli ya Maandalizi ya Tasani, kule Makunduchi, ambayo (ujenzi na samani za ndani) itatugharimu Sh. Mil. 600 hadi itakapokamilika Disemba mwaka huu, ili kuruhusu watoto wa maeneo jirani kuanza masomo Januari 2024,” alibainisha Bi. Zaipuna.
Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu huyo alimpongeza Rais Samia kwa wazo chanya lililozaa Tamasha la Kizimkazi, ambalo limekuwa mhimili na chachu ya miradi mbalimbali ya maendeleo endelevu ya kielimu na kiuchumi miongoni mwa Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla wake.
Kwa upande wake, Rais Samia aliipongeza NMB sio tu kwa ushiriki endelevu wa kufanya miradi ya maendeleo kwa miaka kadhaa, bali pia kwa kusapoti Serikali kupitia tamasha hilo, ilikofanya mambo muhimu kwa ustawi wa Wazanzibar kielimu na kiuchumi, mwaka huu kupitia miradi yao miwili ya Skuli ya Maandalizi Tasani na Tawi jipya la NMB Paje.
“Ahsanteni wadau wote wa maendeleo mliofanya uwekezaji mkubwa katika Sekta za Elimu na Uchumi. Shukrani kwa NMB ambayo inagharamia ujenzi wa Skuli ya Maandalizi Tasani, ambako nimeweka Jiwe la Msingi juzi, tayari kwa ujenzi unaoenda kutoa elimu ya awali kwa watoto wetu wa Makunduchi.
“Jana, nimezindua Tawi jipya NMB Paje na kitu cha kufurahisha ni kuona licha ya uchanga wa tawi, lakini kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wateja.
“Na habari njema kwa wote ni kuwa na mimi ni mteja wa NMB, ingawa nimekuwa hivyo kwa muda mrefu kabla hata ya ufunguzi huu wa jana,” alisisitiza Rais Samia na kuzidi kuipongeza NMB na taasisi kadhaa za fedha kwa udhamini endelevu kwa miaka mingi ya tamasha hilo.