Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) akiwemo Mkurugenzi wa COSTECH Dkt. Amos Nungu wakati wakikabidhi Hundi Sh. 1, 290, 000, 000 kwa wanufaika kwa makundi wa utafiti kwa ajili ya kufadhili miradi ya utafiti katika katika hafla ya kuhitimisha mafunzo na utoaji Tuzo kwa Watafiti Wanufaika wa Mradi wa Utafiti iliyofadhiliwa COSTECH ambapo imefanyika leo
Septemba 1, 2023 Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo
akizungumza jambo leo Septemba 1, 2023 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuhitimisha mafunzo na utoaji Tuzo kwa Watafiti Wanufaika wa Mradi wa Utafiti iliyofadhiliwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Mkurugenzi wa COSTECH Dkt. Amos Nungu akizungumza jambo leo Septemba 1, 2023 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuhitimisha mafunzo na utoaji Tuzo kwa Watafiti Wanufaika wa Mradi wa Utafiti iliyofadhiliwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Baadhi Watafiti kutoka Taasisi mbalimbali, wafanyakazi wa COSTECH pamoja na wadau wakiwa katika hafla ya kuhitimisha mafunzo na utoaji Tuzo kwa Watafiti Wanufaika wa Mradi wa Utafiti iliyofadhiliwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
……
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetoa Tuzo ya Sh. 1, 290, 000, 000 kwa wanufaika kwa makundi wa utafiti kwa ajili ya kuifadhili miradi mbalimbali ya Utafiti katika sekta afya, elimu, kilimo, uvuvi pamoja na manunuzi.
Akizungumza leo Septemba 1, 2023 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuhitimisha mafunzo na utoaji Tuzo kwa Watafiti Wanufaika wa Mradi wa Utafiti iliyofadhiliwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, amesema kumekuwa na miradi ya utafiti na ubunifu inayofadhiliwa kupitia COSTECH pamoja na kupitia hatua mbalimbali za tathmini ili kubaini miradi ya kimkakati na inayolenga kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.
“Serikali inajua umuhimu wa utafiti na itaendelea kuboresha mazingira ya utafiti ikiwemo kutoa ruzuku kwa watafiti miaka ili kuleta tija kwa Taifa” amesema Prof. Nombo.
Amesema kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu kwa kuboresha mazingira ya utafiti na ubunifu nchini ikiwemo kugharamia pamoja na kutoa ruzuku kwa miradi mbalimbali ya Utafiti.
Prof. Nombo amesema kuwa serikali inaamini kupitia tafiti na ubunifu inasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya Afya, uchumi pamoja na kijamii.
“Serikali imeongeza rasilimali fedha na kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuvutia wadau ndani na nje ya nchi kuwekeza katika utafiti na ubunifu, kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yamevutiwa na kuongeza washirika wa maendeleo wanaochangia katika shughuli za utafiti na ubunifu nchini” amesema Prof.Nombo.
Amefafanua kuwa katika kipindi Cha miaka mitano (2019-2022), serikali kugharamia jumla ya miradi 49 ya utafiti, iliyojumuisha zaidi ya watafiti 235 kutoka Taasisi za Elimu ya Juu na zile za Utafiti na Maendeleo nchini.
Amesema kuwa katika kipindi Cha miaka mitano serikali imetumia Shilingi bilioni 9.04 kwa Taasisi 11 za Elimu ya Juu na Utafiti ambazo zimewezesha kukarabati na kununua vifaa vya maabara za utafiti na miundombinu mingine.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu, amesema kuwa hivi karibu wamepokea mapendekezo ya mradi wa utafiti 92 baada ya kupitia wamefanikiwa kupitisha miradi saba kulingana na bajeti iliyopo.
Amesema kuwa miradi hiyo saba ya utafiti zimejikita katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, elimu pamoja na manunuzi.
“Timu ya Costech imekaa na watafiti kwa muda wa siku tatu kwa ajili kutoa mafunzo ya kutegeneza mpango kazi ya miradi yao ili iweze kuwa uhalisia katika utendaji wake” amesema Dkt. Nungu.
Amesema kuwa katika siku hizo tatu watafiti wameweka mikakati ya kutekeleza tafiti ambazo zimefadhiliwa na Costech.
Hata hivyo Dkt. Nungu amebainisha kuwa kupitia wafadhili mbalimbali katika kipindi cha miaka mitatu COSTECH imefanikiwa kuleta shilingi bilioni 9 nchini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya utafiti.
Dkt. Nungu amesema kuwa fedha hizo zimetumika katika kufadhili miradi mbalimbali utafiti ya viwanda ikiwemo Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Ameeleza kuwa miradi mengine imetekelezwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO).
“Natoa wito kwa vyuo vya elimu ya juu vya utafiti kuleta mapendekezo ya mradi mpya kwa ajili ya usalama wa chakula ambapo imelenga kuwapatia ufadhili wakimama wanaofanya tafiti” amesema Dkt. Nungu.
Hata hivyo Watafiti hao akiwemo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Neema Lymo, amesema kuwa kuna miradi miwili ya utafiti ambayo imelenga kutatua changamoto katika sekta ya mifugo na uvuvi pamoja na kilimo.
Amesema kuwa kuna changamoto ya magonjwa ambayo yanaathiri mazao, mifuko na kuleta hasara kwa mkulima na mfugaji.
“Kiwango cha uzalishaji wa chakula kinapungua pamoja na kukosekana kwa upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wakati ikiwemo masoko, mbegu” amesema Bi. Lymo.
Bi. Lymo ameleeza kuwa katika kutafuta majibu ya changamoto hizo timu ya SUA kwa kushiriki na Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali wameleta mifumo miwili ambayo itakwenda kusaidia kutatua tatizo hilo.
Amesema kuwa mifumo yote miwili inatumika teknolojia ya kisasa ambapo wa kwanza utatusaidia kugundua magonjwa ya kilimo na mifumo kwa wakati.
Mfumo wa pili utasaidia kuwaunganisha wadau mbalimbali ikiwemo wakulima, wafungaji pamoja na watu wa masoko jambo ambalo litakuwa na tija kwa Taifa.
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo, Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Daktari Bigwa wa Magonjwa ya Akili Dkt. Innocent Mwambeki, amesema kuwa wamekuja na teknolojia katika kuongeza ufanisi kwa huduma ya afya ya akili pamoja na kuongeza utambuzi wa magonjwa ya akili nchini.
Dkt. Mwambeki amesema kuwa mradi huo unatumia akili bandia kwani katika magonjwa ya akili kuna changamoto ya kutofahamu, kuchelewa watu kupata huduma, ukosefu wataalamu wa kutosha wa kutoa huduma pamoja na ukosefu wa teknolojia.
“Teknolojia hii inamuwezesha mtanzania wa kawaida kutambua afya yake ya akili na kuweka kujua umuhimu wa kupata huduma mapema pamoja na kumsaidia Daktari kutambua magonjwa ya akili na kufanya maamuzi ya Tiba” amesema Dkt. Mwambeki.
“Mradi huu unatekelezwa na taasisi tatu za kitafiti ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na tumefadhili na Costech, tunategemea kuanza mapema mwezi Oktoba, 2023 na kumaliza ndani ya mwaka mmoja na nusu” amesema Dkt. Mwambeki.