Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi Benki ya CRDB pamoja na wadau mbalimbali wakati wa hafla ya Uzinduzi wa kuuza hati fungani uliyofanyika leo Agosti 31, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akizungumza jambo katika Uzinduzi wa hati fungani za Benki ya CRDB uliyofanyika leo Agosti 31, Jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya CRDB Groups, Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa ufafanuzi katika hafla ya Uzinduzi wa kuuza hati fungani za Benki ya CRDB uliyofanyika leo Agosti 31, Jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemus akizungumza jambo katika Uzinduzi wa hati fungani za Benki ya CRDB iliyofanyika leo Agosti 31, Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Groups, Dkt Ally Laay akizungumza jambo katika Uzinduzi wa hati fungani za Benki ya CRDB iliyofanyika leo Agosti 31, Jijini Dar es Salaam.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezitaka taasisi za fedha nchini kuwa wabunifu kama Benki ya CRDB kwa kutoa fursa kwa watanzania kuwekeza kwa kununua hati fungani yenye thamani ya dola za Marekani milioni 300 zitakazowekezwa kwenye miradi yenye malengo wa kulinda mzingira nchini Tanzania.
Akizungumza leo tarehe 31/8/2023 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya Uzinduzi wa mauzo ya hati fungani,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amesema kuwa watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa kwa mtu binafsi, kampuni, taasisi pamoja na Mashirika mbalimbali ndani na nje ya Nchi.
Prof. Mkumbo amesema kuwa hati fungani inakwenda kuisaidia serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na bajeti yake.
“Benki ya CRDB inakuwa ya kwanza katika hatifungani hii ni ya kihistoria sio tu katika sekta ya fedha nchini bali nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni hatifungani itakayowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira na yenye matokeo chanya kwa jamii yaani green, social and sustainability bond” amesema Prof. Mkumbo.
Amesema kuwa uuzaji wa hatifungani ni hatua muhimu katika ustawi na maendeleo ya uchumi nchini kwani utachangia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha yaani National Financial Sector Development Master Plan 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya miradi katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.
“Mkifanikiwa kuuza hatifungani hii na mimi nitakuwa nimefanikiwa kwani nikienda kwa Mhe. Rais kumpa ripoti ya uwekezaji sitaacha kusema kuhusu hatifungani hii” amesema Prof. Mkumbo.
Amefafanua kuwa riba inayotolewa katika hati fungani ni asilimia 10.25 ambayo ni kubwa na rafiki kwa wote watakaonunua.
Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya CRDB Groups, Bw. Abdulmajid Nsekela, amesema kuwa wapo tayari kutoa ushirikiano kwa taasisi ya fedha kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika kufanikisha hatua fungani.
Bw. Nsekela amesema kuwa uamuzi wa kutoa hatifungani umetokana na mahitaji makubwa ya mikopo pamoja na mwelekeo wa dunia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Athari za mabadiliko ya tabianchi zimezigusa jamii nyingi duniani, hivyo kulazimu kuunganisha nguvu za kukabiliana nazo” amesema Bw. Nsekela.
Amesema kuwa mafuriko, ukame na mlipuko wa magonjwa ni baadhi ya matokeo ya mabadiliko haya ya hali ya hewa ambayo hatifungani ya kijani inakusudia kuwezesha miradi ya kukabiliana nayo.
Ameleeza kuwa nchi nyingi duniani zinatoa hatifungani hivyo wakati umefika kwa kila mtanzania kujitokeza kuwekeza ili kwa pamoja katika tuyalinde mazingira.
“Hati fungani hii inaaza kuuzwa leo katika matawi yote ya Benki ya CRDB hadi Oktoba 6, 2023, pia unaweza kuingia katika website ya CRDB kwa ajili kujaza fomu ya maombi” amesema Bw. Nsekela.
Amesema kuwa hatifungani hiyo ya miaka mitano itauzwa kwa awamu huku awamu ya kwanza Benki ya CRDB inakusudia kukusanya mpaka shilingi 55 bilioni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Groups, Dkt Ally Laay ametoa pongezi kwa Mamlaka zote ambazo zimeusika katika kufanikisha jambo hilo muhimu.
Amesema kuwa Bara la Afrika ni bara linaloathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi ingawa lenyewe linachangia kwa kiasi kidogo sana uchafuzi na uharibifu wa mazingira.
“Wakati wote Benki ya CRDB imekuwa mfano wa kuleta bidhaa bunifu sokoni zinazosaidia kutatua changamoto za wateja wake na jamii nzima kwa ujumla kwa hatifungani na inaendelea kuonyesha mfano,” amesema Dkt Laay.
Afisa Mtendaji Mkuu wa
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemus Mkama ameipongeza Benki ya CRDB kwa kufanikiwa kuitoa na kuiuza hatifungani hiyo inayokidhi vigezo vya kimataifa vya hatifungani za kijani.
“Ni matumaini yangu kwamba miradi mingi ya kimazingira itanufaika na fedha zitakazotokana na mauzo ya hatifungani hii. Nitumie fursa hii kuzihamasisha taasisi nyingine za fedha, mashirika ya umma na kampuni binafsi kutoa hatifungani zitakazosaidia kufanikisha maendeleo ya taifa letu,” amesema CPA. Mkama