Taasisi ya Global PeaceWomen kwa kushiriki na Global Peace Foundation Tanzania kupitia mradi wa Mama hodari Initiative imewajengea uwezo kiuchumi wahitaji wakiwemo wakinamama wenye ulemavu wanaolea watoto pekee yao (Single Mothers) katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.
Mradi huo wa Mama hodari Initiative umefanikiwa kuwasaidia wasiwe tegemezi katika jamii na kuweza kutunza watoto na familia zao kwa ujumla wakiwa na amani kuanzia nyumbani.
Wanufanika na mradi huo ni Kuruthum Mohamed ambaye anafanya kazi ya kutengeneza makapu, Ngano Abdallah mfanyabiashara ndogo ndogo za kuuza karanga, mkaa wa kupima ambapo wote wana ulemavu wa viungo.
Wengine ni Husna Abdulahman mfanyabiashara wa kuuza samaki wabichi, Hajra Rashid ambaye anauza chakula ufukweni ambapo wote ni Albino.
Mradi umefanikiwa kuwapatia mafunzo muhimu ya ujasiriamali katika masuala ya Usimamizi wa Fedha, Ubunifu, Kufanya biashara kidigitali, Kutafuta masoko ya biashara zao.
Pia wamejengewa uwezo wa kufanya biashara kama kikundi na mbinu za kuomba mikopo katika taasisi mbalimbali ikiwemo halmashauri na ofisi ya Waziri Mkuu.
Licha ya mafunzo wanaendelea kushiriki programu ya unasihi (mentorship) ambapo wanaunganishwa na wataalamu mbalimbali ndani na nje ya Wilaya ya Kilwa ambapo wanaendelea kuimarika na kuweza kusimama kiuchumi.
Hata hivyo, mradi umechangia kuwapa fedha ya mtaji (kiasi cha shilingi milioni moja na laki mbili taslimu) wakina mama hao kwa kufanya biashara ya kikundi (kuuza samaki ndani na nje ya Kilwa Masoko).
Wakina mama hao kwa sasa wanafanya biashara zao binafsi na kikundi kwa utaratibu na ubunifu unaoendana na mazingira yao tofauti na awali ambapo walikuwa wanafanya biashara kwa mazoea.
Baada ya kupata mafunzo kwa sasa wanatunza fedha Benki na M-KOBA badala ya kuweka ndani kwenye kibubu pamoja na kutunza kumbukumbu za mapato na matumizi, faida, hasara katika biashara zao nk.
Kwa sasa wamepiga hatua kwani wamefanikiwa kuajiri kijana wa kuwasaidia kwenda kuchukua mzigo wa samaki na kuuza ndani na nje ya Kilwa Masoko.
Wamezidi kujitegemea na kuweza kujikimu mahitaji muhimu yao binafsi na watoto wao ikiwemo kulipia huduma ya hospitali, kununua vifaa vya shule, kulipia bili ya chakula, maji, mavazi na kuwa tofauti na awali ambapo walikata tamaa na kujiona hawafai na hawana faida katika familia na jamii yao.
Licha ya mafanikio hayo, wakina mama hao bado wanapitia changamoto kubwa ya vitendea kazi vya kurahisisha mizunguko yao ya kila siku katika kuchakarika kulisaka tonge.
Mfano wanatembelea baiskeli za viti mwendo ambapo wanapata changamoto kwani baiskeli hizo kwa sasa haziendani na mazingira waliyopo kwani wanapita njia zenye michanga mingi, hivyo huwapelekea maumivu makali ya kifua hata wakati mwingine kujiuguza na kushindwa kuendelea na na majukumu yao.
Wanahitaji wafadhili wa kuwasaidia baiskeli zenye mota/gia kadri ya mazingira yao au/na bajaji ili iwasaidie mwendo pamoja na kufanya biashara.
Wakinamama wenye ualbino kilio chao kikubwa ni vifaa kama mafuta ya kujikinga na jua, kofia, miwani vya kutosha kwani ili waweze kuingiza chochote hawana budi kuzunguka sana juani kila uchwao, pamoja na vifaa kama friji/friza au/na madeli makubwa ili waweze kutunzia na kusafirisha biashara yao ya samaki kwa masafa ya mbali zaidi nje ya Kilwa Masoko.
Licha ya ushirikiano baina ya Global Peace Women, Global Peace Foundation na serikali ngazi ya Wilaya katika kuwasaidia wakina mama bado juhudi za makusudi kutoka kwa wadau mbalimbali zinahitajika ili kuhakikisha wanatua mzigo wa utegemezi.
Wamedhihirishia kuwa watu wenye ulemavu wa viungo na ualbino sio kikwazo cha kufanikiwa bali nia thabiti na malengo makini na nguvu ya pamoja baina ya watu waliopikwa vizuri na kiu ya kufikia kilele cha maendeleo binafsi na familia kwa ujumla.